

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameungana na Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa, na Rais wa Botswana, Mhe. Duma Boko, katika Mkutano wa Kwanza wa Uwekezaji wa Maji Afrika uliofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini.
Mkutano huo, ulioratibiwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini na Jopo la Ngazi ya Juu la Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika (Africa Water Investment Programme – AIP), umebeba dhamira ya kuhamasisha na kuongeza uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji barani Afrika.
Viongozi hao watatu, pamoja na wakuu wengine wa nchi, mawaziri, wawekezaji na wadau wa maendeleo, wanajadili mbinu na sera za kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama, kuongeza miundombinu ya maji, pamoja na kulinda vyanzo vya maji ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji inayoikabili Afrika.
Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huu ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji inayolenga kufanikisha ajenda za maendeleo endelevu, kukuza uchumi wa kijani na kuboresha maisha ya wananchi barani kote.

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!