

Benki ya Absa Tanzania Yatangaza Washindi wa Wazo Challenge Tanzania 2025
• Biashara tatu bora za FinTech zachaguliwa kutoka kwa kumi bora waliofika fainali miongoni mwa maombi 94 yaliyopokelewa
• Washindi watapata zawadi ya kifedha, msaada, fursa ya kuonekana, na nafasi ya kutekeleza suluhisho zao na Benki ya Absa Tanzania
• Hitimisho la safari ya ubunifu na hackathon ya siku 60 kwa ushirikiano na Hindsight Ventures
Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na Hindsight Ventures leo imetangaza washindi watatu bora wa shindano la kwanza kabisa la Wazo Challenge Tanzania katika hafla ya Demo Day iliyofanyika kwa shamrashamra jijini Dar es Salaam. Demo Day imehitimisha safari ya ubunifu na ujenzi wa biashara ya siku 60, ikiangazia vipaji bora vya FinTech kutoka Tanzania.

Biashara tatu zilizoshinda – Ghala, Black Swan, na GrupBuy – zimeibuka kutoka kwa kundi la kumi bora waliowasilisha suluhisho zao za kisasa za benki za kidijitali mbele ya jopo la majaji lililojumuisha wataalamu kutoka Benki ya Absa Tanzania na Hindsight Ventures. Startups hizi zimeonyesha ubunifu wa hali ya juu, umuhimu wa suluhisho zao, na uwezo wa kukua, hivyo kupata nafasi ya kutekeleza suluhisho zao kwa ushirikiano na Benki ya Absa Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Obedi Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, alisema: “Kwetu Absa, tunaamini kuwa kila stori ina thamani. Wazo Challenge Tanzania imetengeneza jukwaa la kusimulia hadithi za ubunifu, maono, na mabadiliko kutoka kwa FinTechs bora kabisa za Tanzania. Mpango huu unaakisi kusudi letu – Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja… stori moja baada ya nyingine. Tunajivunia kuwa sehemu ya safari yao na kusaidia kuyafanya mawazo haya kuwa halisi katika dunia ya huduma za kifedha.”

Bw. Sam Mkuyu, Mkuu wa Huduma kwa Wateja na Kidijitali wa Benki ya Absa Tanzania, aliongeza: “Tulibuni Wazo Challenge ili kugundua na kusaidia FinTechs zenye uwezo wa kufanya mageuzi makubwa yanayolingana na mahitaji ya mteja wa kidijitali wa kisasa. Tumefurahishwa na ubunifu mkubwa na uwezo wa washiriki wote. Absa itaendelea kuwa chachu ya uvumbuzi na kushirikiana na vipaji vya teknolojia vya ndani ili kubadilisha sura ya huduma za kibenki nchini Tanzania.”
Bw. Ajay Ramasubramaniam, Mwanzilishi Mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Hindsight Ventures, alisema: “Demo Day ya leo ilikuwa ni sherehe ya maono, juhudi, na ubunifu wa kiteknolojia. Ubora wa mawazo yaliyooneshwa na wabunifu kutoka Tanzania umetuthibitishia uthabiti wa mfumo huu wa ubunifu. Tunafurahia kuendeleza ushirikiano wetu na Benki ya Absa Tanzania ili kuwawezesha wajasiriamali wa ndani na kuwafungulia fursa za kimataifa.”

Wazo Challenge Tanzania, yenye kaulimbiu “Benki ya Baadaye”, iliwaunganisha wabunifu wa FinTech kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuchunguza mada kama vile uzoefu wa mteja, utambulisho wa kidijitali, na bidhaa za kwanza za kidijitali. Washiriki wa fainali walipata fursa ya kufaidika na ushauri, msaada wa kiufundi, mitandao ya kimataifa ya FinTech, na bidhaa za teknolojia zenye thamani ya zaidi ya USD 600,000.
Shindano hili ni hatua muhimu katika mkakati wa ubunifu wa miaka mingi wa Benki ya Absa Tanzania na linathibitisha dhamira ya benki hiyo ya kuwezesha mustakabali wa kidijitali wa Afrika kupitia ushirikiano wa kimkakati na suluhisho jumuishi za kifedha.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!