

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti, Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika, (NIMCA) Ernest Sungura amesemaTanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabaraza ya Habari Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 14 hadi 17 Julai 2025.
Mkutano huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Akizungumza katika kipindi cha Front Page kinachorushwa na Global tv na +255Global Radio leo Juni 26M, 2025 Sungura amesema Mgeni Rasmi aliyealikwa kufungua mkutano huo wa kimataifa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amealikwa kushiriki kwa nafasi ya Mgeni Maalum wa mkutano huo na kushuhudia tuzo mahsusi za miaka thelethini (30) ya Baraza la Habari Tanzania.
Sungura ameongeza kwamba mgeni mwingine mashuhuri ni Naibu Mkurugenzi Mkuu, Mawasiliano na Habari wa UNESCO, Dkt. Tawfik Jelassi; huku tukitarajia baadhi ya mawaziri wa sekta ya habari na mawasiliano kutoka katika mataifa ya Afrika kuhudhuria.
Mawaziri hao ni pamoja na William Kabogo Gitau, Waziri wa Habari na Uchumi wa Kidijitali, Kenya,Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tanzania.
Wengine ni Jerry Silaa, Waziri wa TEHAMA, Tanzania, Dkt. Chris Baryomunsi, Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa Kitaifa, Uganda, Cornelius Mweetwa (MB), Waziri wa Habari na Utangazaji, Zambia, Pamoja na Veronica M. Nduva, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Sungura amesema mkutano huo unaandaliwa kwa mara ya kwanza na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (Network of Independent Media Councils of Africa—NIMCA), Umoja wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (East Africa Press Councils-EAPC), na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kama mshirika mahususi.
Aidha, amesema mikutano mingine ya kimataifa itafanyika sambamba na mkutano huo, kama vile, mkutano wa East Africa Press Councils (EAPC), na World Association of Press Councils (WAPC).
Sungura amesema watu zaidi ya mia tano wanatarajiwa kushiriki ambapo mia moja hamsini watatoka nchi mbalimbali duniani. Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu: “Advancing Media and Communication Regulations for Journalism Excellence in Africa” inayotafsiriwa kama “Uboreshaji wa Sheria za Habari na Mawasiliano kwa Ajili ya Umahiri wa Uandishi wa Habari Afrika”.
Kimsingi, mkutano huu ni wa mambo matatu makubwa katika siku tatu muhimu ambayo ni Kwanza: mijadala ya kitalaamu kuhusu changamoto mbalimbali zinazoathiri tasnia ya habari na namna mabaraza ya habari kote duniani yanavyokabiliana na changamoto hizo.
Pili: maonesho ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari, taasisi za umma na binafsi na tatu: Uzinduzi wa maadhimisho ya miaka thelathini (30) ya Baraza la Habari Tanzania, ambapo wanachama wa MCT, wengi wao vyombo vya habari, taasisi za kihabari na vyuo vya uandishi wa habari watakuwa wakikumbuka na kujifunza jinsi gani walivyomudu kuzingatia weledi na maadili ya tasnia ya habari kwa kujisimamia.
Na Elvan Stambuli GPL
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!