
Chama cha ACT Wazalendo kimewasilisha rasmi maelezo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kikiweka wazi msimamo wake kuhusu malalamiko yaliyotolewa na Katibu Mwenezi wa chama Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Joseph Ndala, kupinga uteuzi wa Luhaga Joelson Mpina kama mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2025.
Malalamiko hayo yalitolewa kupitia barua ya tarehe 14 Agosti 2024, ambapo Monalisa, ambaye pia ni Naibu Waziri Kivuli wa Sanaa, Utamaduni na Michezo katika Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT-Wazalendo, alidai mchakato wa uteuzi wa Mpina ulikiuka Kanuni za chama na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Monalisa alibainisha kwamba Mpina hakukidhi masharti kadhaa, ikiwemo: Kuwa mwanachama wa chama kwa angalau miezi mmoja kabla ya uteuzi, Kutangaza mali zake binafsi na Kuonesha uelewa wa falsafa na sera za ACT-Wazalendo
Aidha, alidai kwamba mabadiliko ya kanuni ya 2024 yanamtaka mgombea kuwa mwanachama kwa siku saba kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa ndani, jambo ambalo kwa mujibu wake, Mpina hakutimiza.
Maelekezo kutoka Ofisi ya Msajili
Msajili wa Vyama vya Siasa, kupitia barua iliyosainiwa na Sisty Nyahoza tarehe 19 Agosti 2025, aliitaka ACT-Wazalendo kutoa maelezo juu ya malalamiko hayo kabla ya tarehe 20 Agosti 2025 saa 9:30 alasiri, kwa kuzingatia ratiba ya uchaguzi iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Msimamo wa ACT Wazalendo
Hata hivyo, vyanzo vya kuaminika ndani ya chama vimesema kuwa hoja za Monalisa hazina msingi kisheria, kwani zinategemea kanuni zilizofutwa. Kanuni za mwaka 2016 ambazo zilikuwa na masharti ya mwanachama kutumikia miezi moja, kutangaza mali, na kuonesha uelewa wa falsafa ya chama, zilifutwa rasmi mwaka 2024.
Badala yake, ACT Wazalendo kwa sasa inatumia:
Kanuni za Uendeshaji za mwaka 2024
Mwongozo wa Uchaguzi wa mwaka 2020
Kanuni hizi mpya zinamtaka mgombea kuwa mwanachama angalau siku saba pekee kabla ya kuanza kwa mchakato wa uteuzi wa wagombea uongozi wa serikali, na sharti lililotajwa na Monalisa lilihusu wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama pekee.
Kwa msingi huo, chama kimeeleza kuwa uteuzi wa Mpina ulifanyika kwa mujibu wa kanuni halali zilizopo, na hivyo hakukuwa na uvunjifu wa masharti yoyote.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!