Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Kilombero Sugar Yazindua Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA Mashuleni

  • 8
Scroll Down To Discover

Morogoro, 28 Agosti: Kampuni ya Sukari Kilombero imezindua rasmi Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA Mashuleni, mradi unaoendeshwa na jamii unaoongozwa na dhamira yake ya thamani-shirikishi ya kujenga jamii inayostawi. Mpango huu unalenga kuzipatia shule za sekondari zinazozunguka Kampuni ya Sukari Kilombero vifaa na ujuzi wa kidijitali muhimu kwa mustakabali wa Ukuzaji ujuzi wa TEHAMA nchini.

Kupitia mpango huu, Kilombero Sugar inatoa kompyuta za mezani 35 na meza 10, pamoja na msaada wa kiufundi kutoka kitengo chake cha TEHAMA, kwa Shule ya Sekondari Nyange (Wilaya ya Kilombero) na Shule ya Sekondari Lyahila (Wilaya ya Kilosa).

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Diana Mwakitwange, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Kilombero Sugar, alisisitiza kuwa mpango huu unaendana na vipaumbele vya kitaifa, vikiwemo Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali 2024/25–2029/30 pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Akili Bandia kwa Elimu, mfumo wa mageuzi unaolenga kubadilisha mazingira ya elimu nchini Tanzania.

 

Kompyuta zilizotolewa, ambazo awali zilitumika kwa shughuli za ofisi, zimeboreshwa kwa kuwekwa programu za matumizi ya msingi ya kompyuta. Uboreshaji huu unaunga mkono Mwongozo wa Kitaifa wa Kidijitali kwa Shule na Vyuo vya Walimu (2025) unaolenga kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu nafuu, ya kuaminika na salama ya TEHAMA kwa ufundishaji na ujifunzaji.

Bw. Victor Byemelwa, Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Wadau, alieleza vigezo vya uteuzi wa shule zilizofaidika: “Tulichunguza utayari wa shule katika kujifunza kwa njia ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na uwepo wa mwalimu wa TEHAMA, chumba cha kompyuta kilichotengwa, na uwezo wa shule kuendana na ajenda ya kitaifa ya elimu ya kidijitali.”

Akaongeza: “Huu ni mpango endelevu. Tutafuatilia matumizi na athari za vifaa tulivyotoa na kutekeleza mpango huu kwa awamu, tukiboresha kadri tunavyopata uzoefu.”

Mheshimiwa Wakili Dunstan Kyobya, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero na Mgeni Rasmi, alisifu mpango huu akisema: “Serikali imejipanga kuimarisha uwezo wa walimu na watendaji wa elimu katika kuunganisha zana za kidijitali kwenye ufundishaji na usimamizi. Tutaendelea kuhamasisha ubunifu, utafiti na ushirikiano katika elimu ya kidijitali ili kukidhi mahitaji ya kiteknolojia na viwanda.”

Aidha, aliwahamasisha wadau wengine kuunga mkono jitihada za Kilombero Sugar katika kuchochea mabadiliko ya kidijitali nchini na kujenga jamii inayostawi.

Bw. Gabriel Lyaluu, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyange, alitoa shukrani akisema: “Mchango huu umekuja kwa wakati muafaka. Sasa tuna vifaa vya kutekeleza kwa vitendo ajenda ya elimu ya kidijitali ya kitaifa.”

Bi. Amina Ally, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lyahila, alionyesha furaha yake: “Nimekuwa nikiota siku zote kujifunza zaidi kuhusu TEHAMA. Kupitia kompyuta hizi, sasa naweza kuchunguza fursa katika nyanja hii na kutumia vyema muda wangu shuleni.”

Mpango huu utaendelea kukua, ukiwezesha shule zaidi katika Bonde la Kilombero ili kusaidia mageuzi ya elimu ya kidijitali nchini Tanzania.



Prev Post KUELEKEA MSIMU MPYA ….FADLU AITILIA NGUMU CAF MAPEMAAH….AFUNGUKA ISHU YA ZNZ……
Next Post Israel inatumia njaa kama silaha ya vita Gaza, katika Dira ya Dunia TV
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook