SIKU chache tu baada ya kupangiwa kucheza dhidi ya Gaborone United ya Botswana, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameichambua timu hiyo, huku akiweka wazi kuwa tayari ameshawatuma watu wake ili kuwapeleleza wapinzani wao.
Akizungumza nchini Misri, ambapo yuko na kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano, Fadlu alisema ameipokea droo iliyofanyika hapa nchini kwa uangalifu, huku akianza mara moja kuichunguza timu ambayo wanakwenda kucheza nayo.
Simba imepangwa kucheza hatua za awali Ligi ya Mabingwa Afrika, ikianzia ugenini dhidi ya Gaborone United kati ya Septemba 19 hadi 21, marudiano yakitarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 26 hadi 29, mwaka huu.
Iwapo Simba itapenya kwenye hatua hiyo, itacheza mechi ya raundi ya kwanza na mshindi kati ya Simba Bhora ya Zimbabwe na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.
“Tutacheza na timu ngumu, tulishawahi kucheza na Jwaneng Galaxy tukaona ugumu wake, sasa tunakwenda na Gaborone United. Kucheza na timu za Botswana si kitu rahisi, ni timu zenye wachezaji wanaopenda kukimbia sana, najua watatupa changamoto, lakini sisi tunajivunia maandalizi yetu na ubora wa kikosi chetu.
“Watu wangu wa uchambuzi wameshaanza kazi mara moja kuanza kuichunguza timu hiyo ili tujue ina nguvu wapi na udhaifu wake ni upi, ingawa kidogo najua baadhi ya taarifa zao, ni timu ambayo haina tofauti sana na Jwaneng Galaxy na Township Rollers,” alisema Fadlu.
Alisema ana uhakika wachezaji wa timu ya Gaborone United watakuja kucheza kwa nguvu kwani wanajua wanapambana na timu kubwa ambayo ni ya tano barani Afrika kwa ubora.
Fadlu alisema kwa sasa anajivunia kuwa na kikosi bora zaidi, chenye wachezaji chipukizi na wazoefu wa michuano mikubwa kama hiyo, pia maandalizi wanayoyafanya ni makubwa yenye hadhi ya michuano kama hiyo.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema kingine wanajivunia pia uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, huku akisema safari hii hawatokubali tena kupelekwa Zanzibar kama msimu uliopita kwenye mechi za nusu na fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nafikiri safari hii hawatotupeleka tena (New Amaan Complex), Zanzibar, hatuhitaji hilo, tunataka tucheze Benjamin Mkapa kwa sababu kila kisichowezekana pale kianawezekana,” alisema kocha huyo.
Simba ilicheza mechi ya nusu fainali Zanzibar dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, Aprili 20, mwaka huu, na kushinda bao 1-0, ambapo kwenye mchezo wa fainali dhidi ya RS Berkane, Mei 25, ilitoka sare ya bao 1-1.
The post KUELEKEA MSIMU MPYA ….FADLU AITILIA NGUMU CAF MAPEMAAH….AFUNGUKA ISHU YA ZNZ…… appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!