
Papa Leo wa XIV na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wamezungumza kwa njia ya simu leo kufuatia wito wa Papa akitaka “kila juhudi kufanyika” ili kufanikisha amani ya kweli na ya kudumu, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Vatican, Matteo Bruni.
Simu hiyo imefuatia wito wa Papa wa kutaka amani nchini Ukraine alioutoa wakati wa hotuba yake ya Regina Caeli kutoka kwenye roshani kuu ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili iliyopita.
Katika hotuba yake baada ya sala ya mchana ya Pasaka, Papa alisema: “Ninabeba katika moyo wangu mateso ya watu wapendwa wa Ukraine,” akisisitiza kwamba “kila juhudi ifanyike ili kufikia amani ya kweli, ya haki, na ya kudumu haraka iwezekanavyo.Wafungwa wote waachiwe huru, na watoto warejeshwe kwa familia zao,” aliongeza kusema.

Papa alikumbusha kwamba tarehe 8 Mei 2025, “janga kubwa la Vita vya Pili vya Dunia” lilimalizika miaka 80 iliyopita, “baada ya kusababisha vifo vya watu milioni 60.”
Aliomba pia kwamba kamwe vita visitokee tena, akitoa maombi maalum kwa Ukraine, Gaza, na kwenye mpaka wa India na Pakistan.
Baada ya mazungumzo yao, Rais Zelensky aliandika katika mtandao wa X kuhusu mazungumzo yake ya kwanza na Papa Leo wa XIV, akisema alimshukuru Papa kwa kuunga mkono Ukraine.
“Tunathamini sana maneno yake kuhusu umuhimu wa kufanikisha amani ya haki na ya kudumu kwa nchi yetu na kuachiliwa kwa wafungwa,” alisema Rais huyo wa Ukraine, akiongeza kwamba walijadili pia kuhusu “maelfu ya watoto wa Ukraine waliotekwa nyara na Urusi.”
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!