

Dar es Salaam, 2 Aprili 2025: Wakazi wa Kata ya Msongola Wilaya ya Ilala jijini Dar wamefanya mjadala mzito wa kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye mitaa wanayoishi chini ya usimamizi wa Kituo cha Mtandao wa Jinsia (TGNP).
Mjadala huo uliongozwa na Mwezeshaji kutoka TGNP, Schola Makwaiya na kwa upande wa serikali uliwakilishwa na Afisa Maendeleo (CDO) wa Kata ya Msongola, Elison Machumbe.
Mkutano huo ambao uliwakusanya wakazi hao kutoka kata hiyo yenye mitaa tisa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia ndani yake kukiwa na ukeketaji, ulawiti, ndoa za utotoni, vipigo, wenza kutelekezana na mengineyo.

Mengine yaliyojadiliwa ni changamoto za huduma za afya ikiwemo viashiria vya rushwa, visirani kwa watoa huduma, dharau, ulevi kazini na mengineyo.
Wananchi hao pia walieleza jinsi migogoro ya ardhi ilivyokithiri kwenye maeneo yao huku viongozi wao wa maeneo wanayoishi wakitajwa kuwa chanzo kikubwa cha migogoro hiyo ambapo miongoni mwake ni kuuza eneo moja kwa watu wawili.

Baada ya mjadala mzito kuhusiana na changamoto zinazowakabili wakazi hao mwezeshaji wa mjadala huo, Schola kutoka TGNP aliwashauri wanajamii hao kutafakari cha kufanya ili kuondokana na kero hizo.
Baada ya mjadala huo baadhi ya mambo waliyoazimia ni pamoja na walezi kushauriwa kuwapa elimu ya kujilinda watoto zao ili kujiepusha mambo yanayoweza kuwaingiza kwa watu wabaya.

Lingine lililoazimiwa ni kuunda timu kwenye kata yao itakayosimamia changamoto hizo na kuwasaidia wasiokuwa na upeo wa kujua sehemu za kwenda kudai haki zao.
Kinamama wa maeneo hayo nao pia wameshauriwa kuacha kuchezea kamari pesa wanazoachiwa kwa matumizi ya nyumbani kwani wengi wao wametajwa kuwa na urahibu wa mchezo huo na kujikuta wakiliwa pesa hizo kuwalaza njaa watoto na familia kwa ujumla.

Akifunga mjadala huo, Afisa Maendeleo wa kata hiyo, Elison Machumbe alisema tatizo lingine ni waathiriwa wengi wa majanga hayo hawajui jinsi ya kwenda kudai haki zao na kuwaambia kuwa kwenye kata hiyo kuna maafisa mbalimbali wa kuwasaidia.
Aliwataja maafisa hao kuwa ni pamoja Polisi Kata, Afisa Ustawi wa Jamii, Afisa wa Dawati la Jinsia pamoja na yeye mwenyewe Afisa Maendeleo ambao wote kwa pamoja wapo kwa ajili ya kushughulikia changamoto zao. HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!