

Dar es Salaam, Mei 3, 2025 – Wakili Peter Kibatala, amesema kuwa mteja wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, yuko tayari kuanza mgomo wa kutokula chakula kuanzia mwanzoni mwa wiki ijayo ikiwa hali ya sasa ya mwenendo wa kesi yake ya uhaini haitabadilika.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kibatala amesema kuwa Lissu anachukua hatua hiyo si kwa ajili ya kupata huruma, bali kuonyesha msimamo wake thabiti wa kudai haki itendeke katika mchakato wa kisheria unaoendelea dhidi yake katika Mahakama ya Kisutu.

“Tundu Lissu ataanza kususia kula chakula. Sio kwa sababu nyingine, bali ni kutaka haki itendeke. Atakapoona haki inacheleweshwa au kuvurugwa, basi hatokula hadi atakapoona mwelekeo sahihi wa kisheria,” alisema Kibatala.
Aidha, Wakili huyo alikosoa vikali utaratibu wa kusikiliza kesi kwa njia ya mtandao, akieleza kuwa mfumo huo umekuwa kikwazo kikubwa kwa ufanisi wa kesi na haki ya mshtakiwa kusikilizwa kwa ukamilifu. Alidai kuwa mara nyingi mawasiliano hukatika, hali inayochangia kupoteza muda na kuathiri haki ya usikilizwaji wa haki kwa uwazi.
“Mfumo wa mtandao unatusumbua. Haki haiwezi kuamuliwa kwa teknolojia inayoyumba. Tunataka wananchi waweze kufuatilia kesi hii moja kwa moja mahakamani, kwani hii ni njia mojawapo ya elimu ya uraia,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Kibatala aliwataka wale wanaotoa matamko ya kuogopesha kuhusu mwenendo wa kesi hiyo, kuwahimiza wachunguzi kukamilisha ushahidi na kuwasilisha kesi mahakamani badala ya vitisho vya mitaani.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!