Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Kuongoza Kongamano la Kwanza la Kodi

  • 41
Scroll Down To Discover

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kwanza la kodi litakalofanyika Mei 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo cha Kodi wakishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa lengo la kuwakutanisha watunga sera, wataalamu wa kodi, wafanyabiashara na watafiti ili kujadili mbinu za kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kwa ajili ya kuongeza mapato ya serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Chuo cha Kodi, Profesa Isaya Jairo, alisema kongamano hilo litatoa jukwaa mahsusi la kuangazia mikakati ya kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari, pamoja na mbinu za kuwahamasisha wajasiriamali walioko kwenye sekta isiyo rasmi kuingia katika mfumo rasmi wa ulipaji kodi.

“Kuna sekta zisizo rasmi kama vile wafanyabiashara wadogo, machinga na biashara za mtandaoni; watu hawa wanafanya biashara lakini wengi hawalipi kodi. Kongamano hili litaonyesha sheria na namna ya kudhibiti ukwepaji wa kodi, pamoja na mbinu za kuzuia uingizaji wa bidhaa hafifu kutoka nje ya nchi na kuhimiza matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi,” alisema Profesa Jairo.

Aliongeza kuwa kongamano hilo linafanyika wakati TRA ikiendelea na mageuzi mbalimbali ya kisheria na kiteknolojia ili kuboresha mfumo wa kodi, licha ya changamoto ya sekta isiyo rasmi ambayo inachangia takribani asilimia 45 ya pato la taifa huku ikihusisha idadi kubwa ya nguvu kazi.

Aidha, Profesa Jairo alitoa wito kwa wananchi kushiriki kongamano hilo ili kutoa mchango wao katika kutengeneza mapendekezo ya sera bora, kuimarisha ushirikiano na wadau na kuchochea uhiari wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya taifa.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Kuongeza Wigo wa Kodi na Kuimarisha Ulipaji Kodi kwa Hiari Tanzania.” Washiriki watajadili mada kuu pamoja na mada ndogo mbili: Kupanua Wigo wa Kodi na Kurasimisha Sekta Zisizo Rasmi, na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi.

 



Prev Post Shindano la cmsa 2025: Fursa Kwa Wanavyuo Kuwekeza Mitaji
Next Post MAGAZETI ya Leo Jumamosi 03 April 2025
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook