
Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imetoa wito kwa wachezaji wa michezo ya kubahatisha nchini kucheza kwa makini na ndani ya uwezo wao, huku ikisisitiza umuhimu wa kuweka mipaka ya matumizi na kutumia mifumo inayosaidia uchezaji salama.
Akizungumza leo Septemba 7, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa Africa Safer Gambling Week 2026, Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe, amesema wiki hiyo inayofanyika kuanzia Septemba 7 hadi 11 inalenga kuongeza uelewa kuhusu michezo ya kubahatisha salama, uchezaji wa kuwajibika pamoja na ulinzi wa wachezaji.

“Wiki hii inalenga kuongeza uelewa kuhusu michezo ya kubahatisha salama, uchezaji wa kuwajibika na ulinzi wa wachezaji. Ni jukumu la pamoja kuhakikisha michezo ya kubahatisha inaendeshwa kwa usalama na uwajibikaji.”
Mbalwe amesema mpango huo unawaleta pamoja wasimamizi wa sekta, waendeshaji, wachezaji, wataalamu, jamii na taasisi mbalimbali kutoka nchi za Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano.
“Ni muhimu kwa wachezaji kutambua uwezo wao wa kifedha, kuweka mipaka ya matumizi, kuchukua mapumziko inapohitajika na kutambua dalili zinazoashiria kuwa uchezaji unaweza kuanza kuleta madhara.”
Mbalwe amesema mchezaji anayebaini kuwa anapata changamoto kutokana na mwenendo wake wa kucheza anapaswa kutafuta msaada mapema na kufahamu maeneo sahihi ya kupata taarifa, ushauri na msaada unaofaa.

“Mchezaji anapobaini kuwa anapata changamoto kutokana na mwenendo wake wa kucheza, ni muhimu kutafuta msaada mapema na kufahamu maeneo sahihi ya kupata taarifa na ushauri.”
Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema GBT inatambua changamoto ya kuwepo kwa michezo ya kubahatisha isiyo halali na isiyosimamiwa, akieleza kuwa wachezaji wanaotumia waendeshaji wasio halali wanaweza kukosa ulinzi na usimamizi unaopatikana katika soko linalosimamiwa.
“Wachezaji wanaotumia waendeshaji wasio halali wanaweza kukosa ulinzi, usimamizi na uwajibikaji unaopatikana katika soko linalosimamiwa.”

Amesema suala la michezo ya kubahatisha isiyo halali na isiyosimamiwa litakuwa sehemu ya mjadala katika Pan-African Webinar utakaofanyika kuelekea mwisho wa Africa Safer Gambling Week 2026.
Mbalwe amesisitiza kuwa Africa Safer Gambling Week si kampeni ya wiki moja inayomalizika Septemba 11, bali ni mwendelezo wa jukumu la wasimamizi wa sekta katika kulinda wachezaji, kuongeza elimu na kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika.
“Africa Safer Gambling Week si kampeni ya wiki moja inayomalizika Septemba 11. Ni mwendelezo wa jukumu letu la kulinda wachezaji, kuongeza elimu na kuimarisha ushirikiano wa wasimamizi wa sekta barani Afrika.”
Kwa Tanzania, Mbalwe amesema GBT itaendelea kuhakikisha maendeleo ya sekta ya michezo ya kubahatisha yanaenda sambamba na ulinzi wa wachezaji na jamii.
“Tunataka kuona maendeleo ya sekta ya michezo ya kubahatisha yakienda sambamba na ulinzi wa wachezaji na jamii, ili kukuza uchezaji wa kuwajibika na kuhakikisha sekta hii inakuwa endelevu.”
Pia amevitaka vyombo vya habari kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kutoa elimu kwa jamii kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu umuhimu wa kucheza kwa makini, changamoto zinazoweza kujitokeza pamoja na maeneo sahihi ya kupata taarifa na msaada.
Mbalwe ameipongeza African iGaming Alliance (AiA) kwa kuanzisha Africa Safer Gambling Week na kuwakutanisha wadau kutoka sehemu mbalimbali za Afrika katika kuendeleza ajenda ya michezo ya kubahatisha salama.
Amesema kauli mbiu ya wiki hiyo ni “Kucheza kwa Makini/Kiasi ni Jukumu la Pamoja,” huku akiwataka wachezaji kuweka mipaka yao, kutambua dalili za changamoto na kutafuta msaada mapema wanapohitaji.
“Kucheza kwa makini au kwa kiasi ni jukumu la pamoja. Tunawahimiza wachezaji kuweka mipaka yao, kutambua dalili za changamoto na kutafuta msaada mapema wanapohitaji.”
The post GBT Yatoa Wito Kwa Wachezaji Kucheza Kistaarabu na Ndani ya Uwezo Wao appeared first on Global Publishers.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!