Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Serikali Ya Tanzania Yaondoa Zuio La Biashara Ya Mazao Na Malawi Pamoja Na Afrika Kusini

  • 19
Scroll Down To Discover

Waziri wa Kilimo, Mohamed Hussein Bashe.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kuondoa rasmi zuio la muda la biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo kati yake na nchi za Malawi na Afrika Kusini, hatua iliyochukuliwa kufuatia mazungumzo ya kidiplomasia yaliyoanzishwa mara baada ya zuio hilo kutangazwa.

Tangazo hilo la kuondoa zuio limetolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein M. Bashe, ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya pande zote tatu — Tanzania, Malawi na Afrika Kusini kuanza mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zilizojitokeza katika biashara ya mazao ya kilimo.

“Tarehe 2 Mei 2025, ujumbe wa Serikali ya Malawi utawasili nchini ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, akiambatana na Mawaziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Kilimo, kwa ajili ya mazungumzo rasmi jijini Dodoma,” amesema Waziri Bashe katika taarifa yake kwa umma.

Kwa upande wa Afrika Kusini, mazungumzo bado yanaendelea kupitia wataalamu wa Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, kwa kushirikiana na mamlaka za afya ya mimea na masoko ya nchi hiyo.

Waziri Bashe ameeleza kuwa, “Kuanzia tarehe 26 Aprili 2025, zuio lote limeondolewa rasmi kwa nchi zote mbili. Tunaamini kuwa majadiliano yanayoendelea yatafikia mwafaka unaoridhisha pande zote na kuimarisha biashara ya mazao.”

Serikali ilitangaza zuio hilo mnamo Aprili 23, 2025, kama hatua ya kulinda maslahi ya wakulima wa Tanzania kufuatia vizuizi vya kibiashara vilivyowekwa na nchi hizo dhidi ya mazao ya Tanzania. Hata hivyo, kwa sasa serikali inaonesha msimamo wa kuendeleza mashauriano ya kidiplomasia na kiufundi kwa ustawi wa sekta ya kilimo.

“Serikali inawahakikishia wakulima na wananchi kuwa uhuru wa biashara utaendelea kuheshimiwa, kulingana na matakwa ya afya ya mimea, rasilimali zilizopo na mahusiano mapana ya kidiplomasia kwa faida ya wote,” amesema Waziri Bashe akihitimisha taarifa hiyo.



Prev Post Camerlengo Farrell Aongoza Ibada Ya Kufunika Mwili Wa Papa Francisko, Kuzikwa Leo -Live Update Video
Next Post Makamu Wa Rais Dkt. Mpango Alivyowasili Roma Kumwakilisha Rais Samia Katika Mazishi Ya Papa Francisko
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook