BAADA ya kutoka suluhu katika mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya Yanga nahodha wa Simba SC, Rushine De Reuck, amesema kiwango walichokionyesha kinawapa matumaini makubwa kuelekea michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Beki huyo ameeleza kuwa licha ya ushindani mkali kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba ilicheza kwa nidhamu, umakini na kuonyesha mpira mzuri uliowapa nafasi ya kuondoka na alama muhimu.
Amesisitiza kuwa kikosi chao kilifanya kazi kubwa uwanjani na kila mchezaji alitimiza wajibu wake ipasavyo.
Akizungumzia mwenendo wa mchezo, De Reuck amekiri kuwa Yanga ni timu kubwa yenye uzoefu na historia, lakini alidai kuwa katika baadhi ya nyakati walionekana kupoteza muda, jambo lililopunguza kasi na ladha ya mchezo.
Hata hivyo, amesema hali hiyo haikuwavunja moyo wachezaji wa Simba ambao waliendelea kupambana hadi dakika ya mwisho.
Ameongeza kuwa mshikamano, ari na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi vilikuwa miongoni mwa mambo yaliyoifanya Simba ionekane imara katika pambano hilo.
“Nawapongeza wachezaji wenzangu kwa kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. Kiwango tulichokionyesha ni ishara nzuri kuelekea michezo ijayo. Kwa timu hii tuliyocheza nayo leo na kama tutaendelea hivi, naamini tutakuwa bora zaidi,” amesema Rushine.
Kwa mujibu wa nahodha huyo, morali ndani ya kikosi ipo juu na kama wataendelea kuimarika, Simba inaweza kuwa tishio kubwa katika mbio za ubingwa pamoja na mashindano mengine wanayoshiriki msimu huu
The post SIMBA IKIKOMAA HAKUNA WA KUTUSIMAMISHA, RUSHINE appeared first on Soka La Bongo.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!