HAKUNA mbabe katika Kariakoo Derby baada ya watani wa jadi, Yanga na Simba kugawana alama mojamoja kufuatia sare ya bila kufungana katika mchezo uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi, ulishuhudia kila timu ikionesha kiwango cha juu, nidhamu ya hali ya juu na tahadhari kubwa.
Licha ya presha na ushindani uliotawala uwanjani, hakuna upande uliofanikiwa kuvunja ukuta wa mwenzake ndani ya dakika 90.
Simba ilionekana kuwa imara zaidi katika safu ya ulinzi, ikiongozwa na mabeki wake tegemeo, Toure pamoja na Rushine De Reuck, ambao walifanya kazi kubwa kuwazuia washambuliaji wa Yanga wasiifikie lango lao kwa urahisi.
Juhudi zao zilimfanya mshambuliaji hatari wa Yanga, Laurindo Dilson Maria Aurélio maarufu kama Depu, kushindwa kuendeleza makali yake ya kufumania nyavu kama alivyofanya katika michezo miwili iliyotangulia kabla ya dabi hiyo.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila timu yoyote kutikisa nyavu. Yanga wakiwa wenyeji wa mchezo huo walijaribu kulisakama lango la Simba kwa kasi na pasi za haraka, huku Simba nao wakijibu mapigo kwa mashambulizi ya kushtukiza yaliyolenga kuwashtua wapinzani wao.
Ndani ya kipindi hicho cha kwanza, timu zote zilionyesha kiu ya ushindi, zikishambuliana kwa zamu na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Hata hivyo, uimara wa safu za ulinzi pamoja na umakini wa makipa ulipelekea juhudi zote kugonga mwamba.
Matokeo hayo yanaacha kila upande ukijivunia pointi moja, huku vita ya ubabe wa Kariakoo ikiendelea kubaki wazi, ikipelekea mashabiki kusubiri kwa hamu pambano lijalo litakaloamua nani hasa atajivika taji la mbabe wa jadi.
The post DEPU AFUNGIWA NJIA,DABI BILA BAO appeared first on Soka La Bongo.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!