KOCHA Mkuu wa Young Africans Sports Club, Pedro Goncalves, ameanza kampeni kubwa kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akiwataka washambuliaji wake kuhakikisha wanamaliza kazi mapema ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Yanga itakuwa nyumbani ikiikaribisha JS Kabylie katika pambano muhimu litakalochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo ni wa maamuzi kwa Wananchi wanaohitaji ushindi ili kujihakikishia tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, maandalizi ya kikosi yanaendelea vizuri huku wachezaji wote wakiwa na morali ya hali ya juu.
Amesema kila mmoja anatambua uzito wa mechi hiyo na dhamira yao ni kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo mbele ya mashabiki wao.
“Siyo tu kufuzu robo fainali, tunahitaji kufuzu kwa kishindo. Kocha (Pedro) anahitaji kuona tunamaliza mchezo ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa kufunga mabao ya kutosha yatakayotupa utulivu kipindi cha pili,” amesema Kamwe.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga inaonekana kuwa imara kuelekea pambano hilo, ikiongozwa na nyota kadhaa akiwemo Clement Mzize ambaye amerejea kutoka majeruhi na tayari alionyesha kiwango kizuri katika mchezo uliopita dhidi ya FAR Rabat.
Wengine watakaobeba matumaini ya mabao ni Prince Dube, Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’, Allan Okello pamoja na Buba Jammeh ambaye anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo.
Kwa ujumla, Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na lengo moja tu , kumaliza kazi mapema, kuwapa furaha mashabiki na kukata tiketi ya robo fainali kwa staili ya aina yake.
The post PEDRO, JS KABYLIE KAZI WANAYO DAKIKA 45 appeared first on Soka La Bongo.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!