Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

NECTA Yavionya Vituo vya Mitihani Vitakavyofanya Udanganyifu Mtihani Kidato cha Nne

  • 6
Scroll Down To Discover

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limethibitisha kukamilika kwa maandalizi yote ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) unaotarajiwa kuanza Novemba 17 hadi Desemba 5, 2025, katika vituo 5,868 vya shule na 813 vya watahiniwa wa kujitegemea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Nov 16,2025 jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Prof. Said Mohamed, amesema maandalizi yamefanyika kwa umakini ili kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na uadilifu.

“Kwa mwaka 2025, jumla ya watahiniwa 595,816 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo 569,914 wa shule na 25,902 wa kujitegemea. Kati ya watahiniwa wa shule, wasichana ni 303,886 sawa na asilimia 53.32, huku wavulana wakiwa 266,028 sawa na asilimia 46.68. Aidha, watahiniwa 1,128 wa shule na 56 wa kujitegemea ni wenye mahitaji maalum, hatua ambayo imeifanya NECTA kuweka miundombinu maalum ya kuwawezesha kufanya mtihani bila vikwazo”,Amesema Prof.Mohamed

Akifafanua umuhimu wa mtihani huo, Prof. Mohamed amesema matokeo yake hutumika katika uchaguzi wa wanaojiunga na Kidato cha Tano na fani mbalimbali za elimu ya ufundi kama afya, kilimo na uhandisi huku akisisitiza kuwa mtihani huo ni nguzo muhimu kwa mustakabali wa kitaaluma wa wanafunzi na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia maandalizi,amesema Baraza limekamilisha maandalizi yote ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mitihani, nyaraka na vifaa kwa halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar. Vilevile, Kamati za Mitihani za mikoa na halmashauri zimetoa mafunzo kwa wasimamizi na kuhakikisha vituo vina usalama wa kutosha. Maandalizi ya watahiniwa wenye mahitaji maalum yamekamilika ikiwemo maandishi ya nukta nundu, maandishi makubwa na muda wa nyongeza kwa mujibu wa miongozo.

Baraza pia limezitaka Kamati za Mitihani kuhakikisha usalama wa vituo na kuzingatia miongozo iliyotolewa ili kuzuia mianya ya udanganyifu huku likitoa wito Kwa wasimamizi, kufanya kazi kwa uadilifu, kutotengeneza mazingira ya upendeleo na kuhakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake bila usumbufu.

Kwa upande wa watahiniwa, Prof. Mohamed amewataka kuzingatia kanuni za mitihani na kuepuka vitendo vya udanganyifu ambavyo vinaweza kusababisha matokeo kufutwa. Ameeleza kuwa walimu wamewajengea msingi mzuri na sasa jukumu liko kwao kufanya kwa bidii na kufuata taratibu zilizoekwa.

Aidha Wamiliki wa shule wametakiwa kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani, huku wakuu wa shule wakikumbushwa kuhakikisha utaratibu wa usimamizi unazingatiwa bila kuathiri uhuru wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mtihani. Baraza limeonya kuwa halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kituo chochote kitakachojihusisha au kusababisha uvunjifu wa taratibu.

Aidha, Baraza limeitaka jamii kutoa ushirikiano katika kipindi chote cha mtihani kwa kuimarisha ulinzi, kudhibiti uingiaji holela maeneo ya shule na kutoa taarifa za viashiria vya udanganyifu. Taarifa hizo zinaweza kutumwa kupitia namba 0759 360 000 au barua pepe ya NECTA.



Prev Post PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 16, 2025
Next Post Rais Dkt. Samia: Watanzania Tuendelee Kuliombea Taifa Lidumu Katika Amani
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook