

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo maalum kwa vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuchuja upya mashitaka yanayowakabili vijana walioshtakiwa kwa makosa ya uhaini kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025.
Akihutubia Bunge leo, Novemba 14, 2025, jijini Dodoma, Rais Samia amesema serikali inatambua kuwa kati ya vijana waliokamatwa, wapo waliojiingiza katika maandamano kwa kufuata mkumbo bila kufahamu uzito wa matendo yao, hivyo hawakudhamiria kufanya uhalifu.
“Ninatambua kuna vijana wengi wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini. Wengine hawakujua wanachokifanya, na wengine walifuata mkumbo tu. Nikiwa kama Mama, naelekeza vyombo vya kisheria kuangalia kwa makini makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa ushahidi wa video uliosambaa mitandaoni unaonyesha wazi kuwa baadhi ya vijana walijikuta kwenye maandamano kutokana na msisimko na ushabiki, bila kutambua madhara yake kisheria.
“Ukiangalia zile clip, unaona vijana wanaingia kwa kufuata mkumbo, wanaimba kwa ushabiki. Naelekeza Ofisi ya DPP kuchuja viwango vya makosa. Wale walioingia bila nia ya kufanya uhalifu waachwe waende kwa wazazi wao,” ameongeza.
Kauli hiyo ya Rais Samia imeonekana kutoa mwanga mpya kwa familia na makundi ya vijana waliokumbwa na operesheni za usalama baada ya maandamano hayo, ikionesha msimamo wa serikali wa kulinda sheria bila kuumiza wasio na dhamira mbaya.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!