

Mamlaka ya mahakama nchini Uturuki imetoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Waziri wake wa Ulinzi, na maafisa wengine 35 wakuu wa jeshi na serikali ya Israel, wakikabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Istanbul, uamuzi huo unahusiana na vitendo vya kijeshi vya Israel katika Ukanda wa Gaza na dhidi ya kundi la kimataifa lililokuwa likijaribu kutoa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina waliokuwa wamezingirwa.
Israel, kupitia msemaji wake wa serikali, imekanusha vikali tuhuma hizo, ikisema kuwa inaendesha vita dhidi ya ugaidi, si dhidi ya raia wa Palestina.
Hatua hii ya kiishara kutoka kwa Uturuki imekuja wakati Marekani ikiendelea kukiri nafasi muhimu ya Ankara katika juhudi za kimataifa za kuwapokonya silaha Hamas na kushirikiana katika kikosi cha amani cha kimataifa kinacholenga kutekeleza mpango wa amani wa Donald Trump kwa Gaza.
Ripoti zinaeleza kuwa uamuzi wa mahakama hiyo umetolewa ndani ya mfumo maalum wa uchunguzi wa uhalifu wa kivita, unaolenga kuchunguza mashambulizi ya Israel dhidi ya raia, hospitali na misafara ya misaada, ikiwemo “Global Solidarity Convoy” iliyoshambuliwa huko Gaza.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema, ingawa hati hiyo haina nguvu za moja kwa moja nje ya mipaka ya Uturuki, ni ishara kali ya kisiasa inayoongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel kuhusu matendo yake ya kijeshi katika Gaza.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!