

Kituo cha sheria na Haki za binadamu nchini Tanzania LHRC, wamelitaka Jeshi la Polisi Nchini Tanzania kumuachia mara moja Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Tundu Lissu anayeripotiwa kukamatwa na kutiwa kwenye kituo cha Polisi Mbinga Mkoani Ruvuma, mara baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara Mbinga Mjini Aprili 09, 2025.
LHRC kupitia kwa Mkurugenzi mtendaji wake Wakili Anna Henga kimeeleza pia kusikitishwa na taarifa za kukamatwa kwa Tundu Lissu na wanachama wengine wa Chama hicho, wakieleza kuwa wanafuatilia kwa ukaribu tukio hilo na kuahidi kuwa wataeleza vyema hatua zitakazochukuliwa na kituo hicho.
LHRC pia imeitaka Polisi ya Ruvuma kumpatia haki zote muhimu Tundu Lissu wakikumbushwa kuwa mikutano ya hadhara na maandamano ni haki ya kikatiba kama ilivyobainishwa chini ya kifungu cha 20 cha Katiba ya 1977 na kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya siasa sura ya 258 R.E 2019.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!