Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Wakili Kibatala Aitaka Serikali Kutoa Taarifa Rasmi Kuhusu Usalama wa Polepole

  • 37
Scroll Down To Discover

Wakili maarufu wa Tanzania, Peter Kibatala, ametoa wito kwa mamlaka za usalama nchini kutumia rasilimali zote kuhakikisha hali ya usalama wa Balozi mstaafu Humphrey Polepole inafahamika na kuwekwa wazi kwa umma, kufuatia taarifa zinazosambaa zikidai kuwa mwanasiasa huyo ametekwa.

Kupitia taarifa ya mawakili wa Polepole iliyotolewa Oktoba 6, 2025, Kibatala amesema mteja wao ni mtumishi wa muda mrefu wa taifa, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, hivyo ni muhimu mamlaka kutoa taarifa rasmi kwa umma wa Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuhusu hali yake.

“Tunazitaka mamlaka za usalama wa raia na mali zao kutumia mbinu na rasilimali zote za umma kuhakikisha, na kisha kutoa taarifa kwa Watanzania na dunia kwa ujumla juu ya hali ya usalama na maslahi ya kisheria ya Balozi (mstaafu) Humphrey Polepole,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Kibatala amesema ofisi yake itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu hatua wanazochukua kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali duniani, kuhakikisha suala hilo linapata majibu ya wazi.

Tamko hilo limekuja muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kuwa linaendelea kufuatilia taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu madai ya kutekwa kwa Polepole, likisema kuwa bado linamsubiri aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa mahojiano.

Kwa mujibu wa Polisi, Polepole alitumiwa barua ya wito kisheria ili kufika kuhojiwa kuhusu tuhuma alizozitoa mtandaoni, lakini hadi sasa hajatekeleza agizo hilo.

Hadi kufikia jana jioni, hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu alipo au hali ya kiafya ya Humphrey Polepole, huku mjadala kuhusu usalama wake ukiendelea kushika kasi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

HECHE AZUNGUMZIA KUTEKWA kwa POLEPOLE na WAKILI KUPIGANA MAHAKAMANI – “HILI ni TUKIO BAYA SANA”..



Prev Post Vodacom Tanzania Yaadhimisha Miaka 25 Ya Huduma Katika Wiki Ya Huduma Kwa Wateja
Next Post Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sebastien Lecornu, Ajiuzulu Wiki Chache Baada ya Kuteuliwa
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook