MAGAZETI ya Leo Ijumaa 28 Machi 2025
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza rasmi upasuaji wa ubongo kwa kutumia ‘roboti’ (Akili Unde).
Upasuaji huo unahusisha kifaa kiitwacho ‘Brain Lab- Neuro Navigation System’ ambacho husaidia wataalamu kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu na kupunguza siku za mgonjwa kukaa wodini baada ya upasuaji huo.
Hayo yamesemwa Alhamisi Machi 27, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua hiyo.
“Kwa mara ya kwanza katika nchi yetu (Tanzania) leo tumefanikiwa kufanya upasuaji wa ubongo kwa kutumia kifaa maalumu ( Brain Lab- Neuronavigation System) ambacho kinamuongoza daktari mpaka kwenye shida ilipo bila kufungua fuvu wala mionzi ya X- Ray” amesema Dk Mpoki
Dk Mpoki amesema kuwa upasuaji huo umeongozwa na daktari bingwa mbobezi mzawa kwa kushirikiana na madaktari kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani na kutoa wito kwa Watanzania wenye matatizo ya ubongo kufika katika taasisi hiyo kupatiwa matibabu.
Mkurugenzi wa upasuaji wa ubongo kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani, Profesa Roger Hartl amewashukuru watumishi wa MOI kwa ushirikiano wao ambao wameendelea kumpatia tangia mwaka 2008 na ameahidi kuendelea kutembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuwapatia mafunzo na kuwajengea uwezo wataalam hao.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!