

Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Amani Golugwa, akiambatana na mawakili wa chama hicho, amewasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Agosti 20, 2025, kupinga barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotangaza kutoutambua uongozi wa chama hicho.
Barua hiyo ya Msajili imeeleza kutotambua uteuzi wa Katibu Mkuu, Manaibu Katibu (Bara na Zanzibar) pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu waliopitishwa na Baraza Kuu la CHADEMA Januari 22, 2025, kwa madai kwamba uteuzi huo haukufuata akidi ya kikatiba. Hoja hizo zilifuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Lembrus Mchome, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Mwanga.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kuwasilisha maombi hayo, Golugwa alisema:
“Msingi wa shauri hili ni kupinga maelekezo ya Msajili na kuiomba Mahakama itoe zuio la kutotekelezwa kwa barua hiyo.”
Mahakama imesema uamuzi wa awali kuhusu maombi hayo utatolewa Agosti 28, 2025 saa 8 mchana.
Ikumbukwe kuwa mvutano huu unahusishwa pia na kesi ya awali iliyofunguliwa na Mchome mnamo Aprili 2025, akipinga mchakato wa uchaguzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA akidai haukufuata akidi ya kikatiba.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!