
Kesi ya madai iliyofunguliwa dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA na Katibu Mkuu wa chama hicho, inayohusu zuio la kufanya shughuli za kisiasa, imeahirishwa hadi Agosti 18, 2025, kwa ajili ya kusikilizwa kwa uamuzi wa maombi ya kutengua zuio hilo.
Shauri hilo, Na. 8323/2025, liliwasilishwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA upande wa Zanzibar, Said Issa Mohammed, na linahusu zuio lililotolewa na Mahakama tarehe 10 Juni 2025, ambalo liliwazuia viongozi wa CHADEMA kufanya shughuli za utendaji pamoja na kutumia rasilimali za chama.
Katika hatua ya hivi karibuni, upande wa walalamikiwa kupitia kwa mawakili wao wamewasilisha maombi ya kutaka zuio hilo litenguliwe, wakidai kuwa lilienda kinyume cha haki ya kikatiba ya kushiriki siasa. Pia wameeleza kuwa wakati zuio hilo linatolewa, hawakuwa na mwakilishi mahakamani baada ya Wakili Jebra Kambole kujitoa, hivyo walinyimwa haki ya kusikilizwa.
Hata hivyo, upande wa wajibu maombi umepinga hoja hizo kwa msingi kuwa walalamikiwa hawakukosa haki ya kusikilizwa, bali walishindwa kufuatilia mwenendo wa shauri hilo kwa uzembe wao wenyewe.
Mahakama imesema itatoa uamuzi kuhusu hoja hizo tarehe 18 Agosti, hatua ambayo itaamua kama zuio hilo litaendelea kuwepo au la.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!