
KIGOMA – Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Inspekta Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Mhe. Balozi Simon Siro, amefanya ziara ya heshima kwa viongozi wa dini mkoani humo kwa lengo la kujitambulisha rasmi na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na taasisi za kidini.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Julai 5, 2025, Balozi Siro alimtembelea Mheshimiwa Askofu Joseph Mlola wa Jimbo Katoliki la Kigoma, na Askofu Jackson Mushendwa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) – Dayosisi ya Magharibi.
Akizungumza katika ziara hiyo, RC Siro alieleza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kudumisha amani, maadili, na mshikamano katika jamii, hivyo ni muhimu kwa serikali kushirikiana nao kwa karibu katika kuwatumikia wananchi.
“Nimeona ni vyema nianze kwa kusalimia na kujitambulisha kwa viongozi wetu wa dini, kwani wao ni nguzo muhimu katika kuhakikisha jamii inaishi kwa amani, mshikamano na maadili mema,” alisema Siro.
Kwa upande wao, Maaskofu hao walimkaribisha kwa moyo mkunjufu Mkuu huyo wa Mkoa na kuahidi kuendeleza ushirikiano na serikali katika kuhakikisha ustawi wa wananchi wa Kigoma unafikiwa kupitia maombi, mafundisho, na mshikamano wa kijamii.
Askofu Mlola alieleza kuwa kanisa linaendelea kuwa mshirika muhimu wa serikali katika utoaji wa huduma za kijamii kama elimu, afya, na ustawi wa jamii, huku Askofu Mushendwa akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano ya mara kwa mara kati ya viongozi wa dini na serikali ili kujenga taifa lenye misingi imara ya maadili.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!