
Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Bwanjai, Missenyi, wamempongeza Evance Kamenge kwa kutimiza ahadi yake ya kuchangia shilingi laki 5 katika maandalizi ya video ya albamu ya kwaya ya kanisa hilo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa albamu hiyo Juni 15, 2025, Kamenge alisema amefanya hivyo kama sehemu ya kutambua mchango wa kanisa hilo katika maisha yake, huku akisisitiza kuwa yupo tayari kuendelea kusaidia jamii yake.
Mwenyekiti wa usharika na Mchungaji Gideon Mwesigwa Kayungi walisema Kamenge ni mfano wa uaminifu na kiongozi mwenye nia ya dhati, wakimtaja kuwa mtu anayestahili kuigwa katika jamii.
Kamenge alieleza kuwa hatua hiyo ni mwanzo tu, akiongeza kuwa anatamani kuona wakulima wa Missenyi wakizalisha zaidi na kupata tija kupitia kilimo, akiahidi kuendelea kupambana na changamoto ya uzalishaji mdogo wa mazao.
Alisema kuwa jina lake linamaanisha matumaini na mabadiliko, na kwamba anaomba maombi ya waumini wakati akijipanga kugombea ubunge katika Jimbo la Missenyi kwenye uchaguzi ujao.
Kamenge amejitolea kushirikiana na wananchi na serikali kuboresha hali ya maisha ya wakulima wa Missenyi na Kagera kwa ujumla, huku akiahidi kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!