Morogoro, Tanzania: Kampuni ya Puma Energy Tanzania imetangaza uzinduzi rasmi wa kituo cha umeme wa jua chenye uwezo wa kilowati 570 katika kiwanda cha tumbaku cha Alliance One Tanzania Tobacco Limited (AOTTL). Mradi huu mkubwa, ulioko takriban kilomita 200 kutoka jijini Dar es Salaam katika eneo la Kingolwira, Morogoro, ni hatua muhimu katika dhamira ya Puma Energy ya kuziwezesha sekta za viwanda Tanzania kwa suluhisho la nishati safi, nafuu, na ya kuaminika.
Kituo hiki cha kisasa kinajumuisha paneli za sola 1,296 na inverter 6 zenye ufanisi wa hali ya juu. Mfumo huu uliounganishwa na gridi ya taifa umetengenezwa kutoa umeme wa kutosha wakati wa mchana kipindi chote cha uzalishaji wa kiwanda kuanzia Mei hadi Oktoba. Mradi huu ni matokeo ya Mkataba wa Ununuzi wa Umeme (PPA) wa miaka 10 ulioingiwa kati ya Puma Energy na AOTTL mwezi Aprili 2024, ambao unahakikisha upatikanaji wa umeme safi na wa kuaminika huku ukipunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa vyanzo vya kawaida vya umeme. Ujenzi ulianza mwezi Machi 2025 na kukamilika haraka mwezi Aprili, huku mfumo ukianza rasmi kazi tarehe 4 Mei 2025.
Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, alisema “Mradi huu wa sola katika kiwanda cha Alliance One ni mafanikio makubwa, si tu kwa Puma Energy bali pia kwa sekta ya viwanda Tanzania. Unadhihirisha dhamira yetu ya dhati ya kutoa suluhisho la nishati safi, nafuu, na ya kuaminika linalowezesha biashara kustawi huku tukichangia katika ulinzi wa mazingira na mustakabali wa taifa letu. Tunajivunia kuwa mstari wa mbele katika mabadiliko haya ya nishati, tukionesha namna ubunifu unavyoweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi sambamba na uwajibikaji wa kimazingira.”
Ikiwa na dhamana ya utendaji wa miaka 30, mfumo huu wa sola unahakikisha ufanisi wa nishati wa muda mrefu na uendelevu wa mazingira. Ni ushahidi thabiti wa maono ya Puma Energy ya kuwezesha sekta ya viwanda Tanzania kupitia suluhisho la nishati safi, bunifu, na imara, kwa ajili ya kukuza uchumi unaokwenda sambamba na utunzaji wa mazingira.
The post Puma Energy Yaanzisha Nishati Safi ya Mradi wa Umeme wa Jua kwa Kiwanda cha Alliance One Tanzania Tobacco Limited appeared first on SwahiliTimes.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!