Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Rais Mstaafu Thabo Mbeki Aitaka Afrika Kuwa na Ajenda Yake

  • 33
Scroll Down To Discover

Rais wa Mstaafu wa Afrika Kusini Thabo akizungumza katika Mkutano wa Kibiashara wa Ngazi ya Juu uliodhaminiwa na AngloGlod Ashanti uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, ameitaka jumuiya ya wafanyabiashara barani Afrika kuweka ajenda yenye mwelekeo wa pamoja na malengo makubwa kuelekea Urais wa G20 wa Afrika Kusini mwaka 2025.
Akizungumza katika Mkutano wa Kibiashara wa Ngazi ya Juu uliofanyika jijini Dar es Salaam, Bw. Mbeki alisisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala muhimu kama mshikamano, usawa na maendeleo endelevu, kwa kuzingatia zaidi maendeleo ya bara la Afrika.
Mbunge wa Bumbuli Januari Makamba akisalimiana na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki wakati wa mjadala wa pamoja na wadau mbalimbali kuhusu mustakabali wa Afrika katika hoteli ya Rotana uliofadhiliwa na AngloGold Ashanti.
Mkutano ujao wa G20, ambao utafanyika Afrika Kusini, unalenga kukabiliana na changamoto zinazohusiana kimataifa ikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa ajira, usawa wa kijamii, mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na nishati, miongoni mwa mengine.
Akizungumza katika mkutano huo — ulioratibiwa kwa pamoja na Taasisi ya Thabo Mbeki na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, na kudhaminiwa na AngloGold Ashanti — Bw. Mbeki alibainisha kuwa, licha ya juhudi mbalimbali zilizofanyika alipokuwa madarakani, sasa ni wakati wa sekta binafsi Afrika kuongoza katika kuunda ajenda ya kiuchumi ya bara hili kimataifa.
Simon Shayo, Makamu wa Rais wa Masuala ya Uendelevu ( Afrika) katika kampuni ya AngloGold Ashanti akiongea mbele ya hadhira akiwemo Rais mstaafu wa Afrika Kusini Mr Thabo Mbeki katika kujadili masuala ya Afrika katika moja za matukio ya Siku ya Afrika 2025 katika hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo, uliofanyika katika Hoteli ya Rotana, Dar es Salaam kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 15 ya Mhadhara wa Siku ya Afrika, uliwakutanisha viongozi wa kibiashara, wawakilishi wa sekta binafsi, wasomi na wanadiplomasia.
Bw. Mbeki aliwasihi washiriki kuunda ajenda ya kiuchumi ya pamoja ya Afrika kwa ajili ya jukwaa la kimataifa.
“Lazima tuwe na mpangilio na kuzungumza kwa sauti moja kuhusu masuala ya msingi.” , alisema huku akiwakumbusha kushindwa kwa Mpango wa Utekelezaji wa Afrika (Africa Action Plan) katika miaka ya nyuma, akitoa wito wa kuandaa mapendekezo ya sera yatakayoongozwa na Waafrika.
“Tulikuwa na juhudi kadhaa katika mikutano ya G8 kushinikiza ajenda ya maendeleo ya Afrika kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe. Sasa, kwa kuwa Umoja wa Afrika ni mwanachama wa G20, tunapaswa kutumia fursa hii kusukuma mbele ajenda yetu,” aliongeza Bw. Mbeki.
Mkutano huo wa G20 unaotarajiwa kufanyika Johannesburg mwezi Novemba 2025, utakuwa wa kwanza kufanyika katika ardhi ya Afrika — jukwaa muhimu la kusukuma mbele maslahi ya bara hili.
Pamoja na Umoja wa Afrika, wanachama wa G20 ni pamoja na Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Korea Kusini, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza, Marekani, na Umoja wa Ulaya.
Wakati wa mkutano huo, washiriki walihimiza mataifa ya Afrika kujielekeza katika kutetea maslahi yao na kuweka njia ya maendeleo inayotegemea rasilimali zao, ikiwa ni pamoja na madini.
Mchumi mashuhuri Profesa Samwel Wangwe alisisitiza hitaji kwa mataifa ya Afrika kurejea katika misingi ya kujitegemea na kutathmini upya nafasi ya Umoja wa Afrika.
Alipendekeza pia umoja wa Afrika, kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja, ulinzi wa rasilimali asilia, uwekezaji katika ujuzi wa ubunifu wa kibiashara, na kuweka mazingira rafiki kwa ukuaji wa uchumi kupitia ushirikiano thabiti kati ya sekta ya umma na binafsi.
Mkutano huo uliopewa kaulimbiu: “Kujenga Mwelekeo wa Pamoja kwa Ajili ya Mkutano wa Urais wa G20 wa Afrika Kusini: Kufufua Uamsho wa Afrika’, ulilenga kuandaa msimamo wa pamoja wa wafanyabiashara wa Afrika kwa majadiliano yajayo ya G20.
Akifungua kikao hicho, Simon Shayo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti, alitoa wito wa mabadiliko katika namna sekta binafsi inavyoshiriki kwenye maendeleo.
“Lazima tuwe zaidi ya wadau wa kiuchumi lazima tuwe wasanifu wa mustakabali wa Afrika,” alisema Shayo, akirejelea mchango wa kampuni yao wa zaidi ya miaka 25 katika sekta ya madini nchini Tanzania.
Lukhanyo Neer, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Taasisi ya Thabo Mbeki, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano unaovuka mipaka ya kitaifa na ya kibiashara.
“Tunahitaji sauti moja ya Afrika katika majukwaa ya kiuchumi ya kimataifa,” alisema.
Balozi John Ulanga wa Tanzania aligusia changamoto kubwa, akisema Afrika inapata theluthi moja tu ya uwekezaji wa miundombinu unaohitajika.
Alipendekeza kuwekeza kwenye miradi ya pamoja ya miundombinu ya bara kama vile mradi wa Cape to Cairo, pamoja na kuweka mifumo ya kusaidia biashara kwa vitendo.
“Utekelezaji lazima uongozwe na wakuu wa nchi lakini ujikite katika uhalisia wa Afrika,” alisema Ulanga.
Balozi Ami Mpungwe alitoa wito wa kufikiria upya mtazamo wa maendeleo ya Afrika.
“Rasilimali pekee si suluhisho — ni msingi tu,” alieleza. Akisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika teknolojia, mitaji, na vipaji, alitaja uwekezaji wa Afrika Kusini nchini Tanzania kama mfano bora wa mafanikio ya ndani ya bara.
Majadiliano katika mkutano huo pia yaligusia sekta muhimu kama vile nishati, biashara, na kilimo. Washiriki walihimiza kubadili mtazamo kutoka kuuza mazao ghafi hadi usindikaji wenye thamani zaidi, wakitaja mazao kama korosho kuwa na fursa kubwa ya kiuchumi.
Uwezeshaji wa vijana na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi pia ulitambuliwa kama nguzo kuu za ukuaji wa uchumi.
Katika hotuba ya kufunga mkutano, Emily Kariuki kutoka Taasisi ya Mbeki Ndlela alikumbusha urithi wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Tunaposhirikiana kama Afrika, hatuzuiliki hata katika majukwaa magumu ya kimataifa,” alisema, akiwahimiza washiriki kudumisha ari hiyo.
Mkutano huo ulimalizika kwa ahadi thabiti ya kujenga jukwaa la pamoja na la kimkakati la wafanyabiashara wa Afrika kwa ajili ya kushiriki katika G20.
Wakati wa majadiliano, AngloGold Ashanti ilithibitisha tena dhamira yake ya kuendelea kusaidia majukwaa kama haya, ikiahidi kuendelea kuwa kichocheo cha maendeleo jumuishi na endelevu barani Afrika.



Prev Post GSM Group Yadhamini Mbio za Marathon za Siku ya Afrika 2025
Next Post MAGAZETI ya Leo Jumapili 25 May 2025
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook