

Dar es Salaam, Tanzania – 15 Agosti 2025: Benki ya Exim Tanzania, moja ya taasisi kinara za kifedha nchini na ukanda huu, leo inaadhimisha miaka 28 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na kaulimbiu ya mwaka huu “Miaka 28 ya Kusonga Mbele Pamoja na Wewe.”
Hafla hiyo, iliyofanyika katika makao makuu ya benki hiyo Exim Tower jijini Dar es Salaam, imewakutanisha wafanyakazi na menejimenti kwa ajili ya kutafakari safari ya benki hiyo tangu ilipoanza mwaka 1997 hadi sasa, safari iliyojaa ubunifu, ukuaji na huduma zinazomtanguliza mteja katika kila hatua.
Maadhimisho haya ni alama kubwa ya mafanikio, yakionesha mabadiliko ya Benki ya Exim kutoka tawi moja pekee, Mtaa wa Samora, jijini Dar es Salaam hadi taasisi ya kimataifa yenye matawi katika nchi za Comoro, Djibouti na Uganda. Safari hii ya ukuaji endelevu ni ushahidi wa uimara wa benki na kujitolea kwake kwa dhati kwa wateja wake. Falsafa ya benki inajengwa juu ya misingi yake mikuu: Uwezo wa Kubadilika, Uhakika, Uadilifu, Utaalamu na Bidii ya Kutosheleza Mahitaji ya Wateja.

Katika hotuba yake kwa wafanyakazi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Jaffari Matundu, akielezea maana ya kaulimbiu ya mwaka huu alisema, “‘Wewe’ katika kaulimbiu hii ni kumbukumbu ya wafanyakazi wetu mahiri, ambao ndio moyo na roho ya benki hii, na pia ni wateja wetu, wanaotuamini na ndoto zao, fedha zao na maisha yao ya baadaye. Tunaposherehekea miaka 28, hatuangalii tu tulichojenga nyuma yetu, bali tunaangalia mbele, kwa yale ambayo bado tunaweza kuyafanikisha pamoja.”
Miaka ya hivi karibuni imekuwa ya mageuzi makubwa ya kiteknolojia kwa Benki ya Exim Tanzania. Mageuzi haya makubwa ni pamoja na kuboresha mfumo wake wa msingi wa kibenki (Core Banking System), hatua iliyofungua huduma bunifu na kuimarisha uwepo wake nchini ili kukidhi matarajio ya wateja.

Aidha, Exim Tanzania imeendelea kuzindua huduma mpya zinazothibitisha msimamo wake kama benki inayoendelea kusonga mbele na wateja wake. Miongoni mwa huduma hizo ni Lipa Chapchap kwa wafanyabiashara na uzinduzi wa huduma ya kifahari ya Elite Banking, hatua zinazoiweka Benki ya Exim kileleni kama benki bunifu zaidi nchini Tanzania.
Hivi karibuni pia, benki ilizindua kampeni ya ‘Kopa KiBoss na Wafanyakazi Loan’ inayowawezesha watumishi wa umma kupata mikopo hadi shilingi milioni 200, kwa muda wa marejesho wa hadi miaka 11 – ya kwanza katika taasisi za kifedha nchini.
Akisisitiza umuhimu wa fikra za kimaendeleo katika sekta ya fedha inayobadilika kwa kasi, Bw. Matundu alisema, “Kwa mifumo na ubunifu tulioanzisha, matarajio ya wateja wetu yapo juu zaidi kuliko ilivyowahi kuwa. Ni jukumu letu kutambua mahitaji yao mapema na kuendelea kujifunza, kukua na kujiboresha ili kwa pamoja tuijenge benki na mustakabali wa kifedha tunaoweza kujivunia.”
Benki ya Exim inavyoendelea na safari yake, malengo yake yako wazi: kuendelea kukua, kupanua wigo wake, kuleta ubunifu na kuboresha huduma kwa wateja, sambamba na kuchangia maendeleo ya sekta ya fedha na taifa kwa ujumla.
Maadhimisho ya miaka 28 ya Benki ya Exim Tanzania ni ushahidi wa safari yake yenye mafanikio, na zaidi ya yote, ni uthibitisho wa kujitolea kwake kwa mustakabali bora wa kifedha kwa Watanzania na ukanda mzima.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!