
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) imemteua Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, akichukua nafasi ya Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye ameteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Uteuzi huo umetangazwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, usiku wa Jumamosi, Agosti 23, 2025, katika makao makuu ya chama hicho jijini Dodoma, saa chache baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk. Migiro, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na pia Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), anakuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya CCM kushika wadhifa wa Katibu Mkuu Taifa, nafasi inayomfanya kuwa mtendaji mkuu wa chama tawala nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya CCM, uteuzi huo unalenga kuimarisha uongozi na maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambapo chama hicho kinatarajia kushiriki kikamilifu katika kampeni na ushindani wa kisiasa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!