

Akizungumza tarehe 31 Julai 2025 wakati wa uzinduzi wa kongani hiyo, Rais Dkt. Samia alisema kuwa jumla ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo, ambapo viwanda saba tayari vimeanza kazi na vingine vitano vipo katika hatua ya ujenzi.
Katika hotuba yake Rais Dkt. Samia amesema kuna fursa kuanzisha biashara ndogondogo na huduma zinazozalishwa na mradi huu, akitaja kuwa ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zitazalishwa kutokana Kongani hiyo ya Viwanda.

“Ninaona uwepo wa malori mengi katika kituo hiki cha Kwala, kutalazimu kuimarishwa kwa haraka huduma kama vile maegesho, karakana, vituo vya mafuta, maduka ya vipuri, maeneo ya kuoshea magari, malazi vyakula na makazi” amesema Rais Dkt. Samia.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, Kaimu Mkurugenzi wa Leseni, Bw. Tawi Kilumile, amesema kuwa BRELA imejipanga kuwa kiunganishi muhimu kati ya Serikali, wawekezaji na wafanyabiashara kwa kutoa huduma za usajili wa biashara na leseni kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa Online Registration System (ORS).
“BRELA ni lango la mafanikio ya biashara nchini. Ili mfanyabiashara aweze kunufaika kikamilifu na fursa hizi, ni lazima ajirasimishe. Huduma zote za usajili sasa zinapatikana mtandaoni kupitia mfumo wa ORS,” amesema Bw. Kilumile.
Kupitia ORS, wateja wanaweza kupata huduma zote kwa urahisi, aidha BRELA ina kituo cha huduma kwa mteja ambapo mteja anaweza kuuliza maswali na kupatiwa majibu papo kwa hapo, hali inayochochea mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
Uzinduzi wa Kongani ya Viwanda Kwala unaashiria hatua mpya ya maendeleo ya viwanda nchini, ambapo ajira zaidi ya 50,000 za moja kwa moja na 150,000 zisizo za moja kwa moja zitazalishwa kutokana na viwanda 200 vitakavyojengwa katika Kongani hiyo ya Viwanda.
BRELA inaendelea kuwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hii kwa kurasimisha biashara zao ili kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!