
Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limethibitisha kuwa limemkamata msanii wa vichekesho, Anastanzia Exavery Mahatane (27), maarufu kama Ebitoke, akiwa katika fukwe za Msanga Mkuu, Mtwara, katika hali inayoashiria kuwa amechanganyikiwa.
Akizungumza leo Agosti 1, 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, ACP Issa Suleiman, amesema kuwa awali mnamo Julai 30, 2025, Ebitoke alichapisha taarifa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, ikiwemo Instagram, akidai kuwa ametumbukizwa shimoni na kwamba kuna watu waliokuwa wakitaka kumuua.
Hata hivyo, kufuatia taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilianzisha uchunguzi wa haraka ambao umebaini kuwa hakuna tukio la utekaji wala shimo kama lilivyodaiwa. Kwa mujibu wa Kamanda Suleiman, Ebitoke amekuwa akiishi Msanga Mkuu tangu Aprili 2025 na alikuwa akihifadhiwa na watu aliokuwa anawafahamu kabla ya kukumbwa na matatizo ya kimaisha.
Tarehe 31 Julai 2025 majira ya saa 11 jioni, Polisi walimkamata Ebitoke katika fukwe hizo akiwa peke yake na katika hali ya kuchanganyikiwa. Hakuonesha dalili za kushambuliwa au kujeruhiwa. Baada ya kumkamata, Jeshi la Polisi lilimpeleka Hospitali ya Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kamanda Suleiman amesema, “Tunaomba ndugu na jamaa wa Ebitoke wafike Mtwara ili kutoa msaada wa karibu au kumchukua ndugu yao.”
Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa linaendelea kutekeleza wajibu wake wa msingi wa kulinda raia na mali zao, huku likisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kutoa taarifa za kweli.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!