

Wawekezaji na watunga sera wa ukanda wa Afrika Mashariki wakutana kuchochea uwekezaji wa mitaji ya ndani kwa ajili ya miundombinu.
Jukwaa lavikutanisha mifuko ya pensheni, taasisi za fedha za maendeleo na wasimamizi wa sekta kutoka Tanzania, Kenya na Uganda.
Stanbic yaongoza juhudi za kuhamasisha mitaji ya ndani kutoka kuwa akiba ya hifadhi kwenda kuwa kichocheo cha uchumi halisi.
Arusha, Tanzania – Jumatano, 23 Julai 2025 – Jukwaa la Wawekezaji wa Taasisi Afrika Mashariki limefanyika kwa siku mbili mjini Arusha kuanzia tarehe 22 hadi 23 Julai 2025, likivuta washiriki kutoka mifuko ya pensheni, taasisi za fedha za maendeleo, watunga sera na wasimamizi kutoka Tanzania, Kenya na Uganda, kujadili namna mitaji ya ndani inaweza kuhamasishwa kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu.
Likiratibiwa kwa pamoja na Stanbic Bank Tanzania, Stanbic Bank Kenya na Stanbic Bank Uganda, jukwaa hili lililenga kuhamasisha mitaji ya ndani kutoka kuwa akiba isiyotumika hadi kuwa uwekezaji wa matokeo katika sekta muhimu kama vile miundombinu, nishati, makazi na miunganisho ya kidijitali. Kwa ushiriki wa wasimamizi wa hazina za taifa, wakala wa usimamizi wa fedha, na taasisi za umma, jukwaa hili linajipanga kuwa juhudi ya pamoja ya kikanda kubadilisha mikakati kuwa miradi inayotekelezeka.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Benedict Nkini, Makamu wa Rais, Taasisi za Fedha – Stanbic Bank Tanzania, alisema jukwaa hilo limekusudiwa kutoa matokeo ya kweli na siyo mijadala ya kawaida. “Hili siyo tu tukio jingine la wataalamu,” alisema Nkini. “Ni jukwaa la kuunganisha mitaji na miradi. Kwa zaidi ya miaka thelathini hapa Tanzania, tumeshirikiana na sekta mbalimbali kuwezesha uwekezaji wenye matokeo. Sasa tunapanua juhudi hizi kuvuka mipaka, kwa sababu changamoto za kikanda zinahitaji suluhisho la kikanda na mitaji ya kikanda.”
Jukwaa hili limekuja wakati kukiwa na wasiwasi kuwa licha ya kuwa na mabilioni katika mitaji ya pensheni na akiba ya ndani ya muda mrefu, nchi za Afrika Mashariki bado zinategemea mno fedha za nje kwa ajili ya miundombinu. Wataalamu wanasema hali hii siyo endelevu, na kwamba tatizo haliko kwenye ukosefu wa fedha, bali ni ukosefu wa miradi inayotekelezeka, kutokuwepo kwa muafaka wa uwekezaji wa mipaka na ukosefu wa sera madhubuti.
Aboubakar Massinda, Makamu wa Rais Mwandamizi, Nishati na Miundombinu Stanbic Bank Tanzania, alisema ukanda huu tayari una rasilimali za kutosha kutatua changamoto zake za miundombinu ikiwa utaweza kufanya kazi kwa pamoja. “Kuna mtaji wa kutosha ndani ya Afrika Mashariki kufadhili maendeleo ya Afrika Mashariki,” alisema Massinda.

“Lakini tunahitaji kuimarisha imani, kuoanisha kanuni na kujenga mtiririko wa miradi inayowekeza, Kenya inaleta uzoefu mzuri katika maandalizi ya miradi, Uganda inaleta uthubutu wa sera, na Tanzania inaleta ukubwa na utulivu. Kwa pamoja, hizi ni fursa kamili na ya kuvutia kwa wawekezaji.”
Katika siku ya kwanza, washiriki walijadili kwa kina namna ya kutambua miradi ya miundombinu inayotekelezeka siyo tu pendekezo kubwa, bali miradi yenye mifumo ya kifedha ya wazi, mbinu za kupunguza hatari, na thamani ya muda mrefu kwa umma. Wataalamu pia walichambua jinsi maandalizi hafifu ya miradi, mazingira ya usimamizi yasiyo thabiti, na mifumo ya ununuzi iliyogawanyika vinavyoendelea kuwakatisha tamaa wawekezaji wa taasisi hasa mifuko ya pensheni.
Mbali na pengo la fedha, washiriki pia walisisitiza umuhimu wa uratibu wa kikanda. Tofauti katika sheria, viwango vya taarifa, na sera za manunuzi kati ya Tanzania, Kenya, na Uganda zimekuwa zikikwamisha juhudi za kutekeleza miradi ya kikanda. Jukwaa hili lilitoa nafasi adimu kwa wasimamizi, taasisi za fedha, na maafisa wa serikali kujadili namna ya kuoanisha mifumo hii bila kuathiri mamlaka za kitaifa.
Ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali pia ulikuwa ajenda kuu, kwa makubaliano kuwa serikali pekee haziwezi kuziba pengo la miundombinu, na sekta binafsi inaweza kushiriki tu pale faida zinapokuwa dhahiri, hatari zinashirikiwa, na muda wa utekelezaji unatarajiwa.
Stanbic Bank, ambayo wiki iliyopita ilitangazwa kuwa Benki Bora ya Uwekezaji Tanzania na jarida la Euromoney, imesema inaingia rasmi katika nafasi ya kuratibu mijadala hii kutokana na uzoefu wake mkubwa katika kuwezesha miamala migumu kwenye sekta mbalimbali.
Waandaaji wa jukwaa wamesema hii ni mwanzo tu, kuwa jukwaa hili ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuhamishia uzito wa uwekezaji wa miundombinu kutoka kwenye masoko ya kimataifa hadi kwenye taasisi za kifedha za Afrika Mashariki.
Jukwaa limevutia ushiriki wa hazina za taifa, mifuko ya pensheni ya kitaifa, taasisi za fedha za maendeleo za kimataifa, na wizara muhimu kutoka nchi zote tatu.
Kwa upande wa Stanbic, ujumbe ni wazi Afrika Mashariki iko tayari kufadhili maendeleo yake yenyewe, na benki hiyo ina nia ya kuwa kiungo muhimu katika mchakato huo wa mabadiliko.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!