
Kamchatka, Russia – WATU 49 wanahofiwa kupoteza maisha baada ya ndege ya abiria aina ya Antonov An-26 kuanguka leo asubuhi, Alhamisi Julai 24, 2025, katika eneo la mashariki ya mbali mwa Russia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali TASS, ndege hiyo inayomilikiwa na shirika dogo la ndege la Angara Airlines, ilipoteza mawasiliano na mnara wa kuongozea ndege muda mfupi kabla ya kutua katika uwanja wa ndege wa Palana, mkoani Kamchatka.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa na watu 49, wakiwemo abiria na wahudumu, waliosafiri kutoka Petropavlovsk-Kamchatsky kuelekea Palana. Mabaki ya ndege hiyo yameripotiwa kupatikana karibu na mwambao wa Bahari ya Okhotsk, huku operesheni za uokoaji zikikumbwa na ugumu kutokana na hali mbaya ya hewa.
Katika taarifa kutoka Kremlin, Rais Vladimir Putin ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuagiza uchunguzi wa haraka na wa kina kufanyika ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
“Tunaungana na familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye tukio hili la kusikitisha,” alisema msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov.
Hii si mara ya kwanza kwa mkoa wa Kamchatka kushuhudia ajali ya anga, huku wadadisi wa masuala ya usafiri wa anga wakiitaka serikali ya Russia kuongeza usimamizi wa kiusalama kwa mashirika madogo ya ndege yanayohudumia maeneo ya mbali yenye changamoto za kijiografia na hali ya hewa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!