Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Rais Dkt. Samia Chifu Hangaya Awa Mtemi Wa Sungusungu Mikoa 5

  • 39
Scroll Down To Discover

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepewa heshima na hadhi ya kuwa Mtemi wa Sungusungu, jeshi la jadi, kwa mikoa mitano ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Tabora.

Mhe. Rais Dkt. Samia ambaye pia ni Mkuu wa Machifu nchini, akijulikana kwa jina la Chifu Hangaya, ametangazwa rasmi kuwa Mtemi wa Sungusungu kupitia risala ya utii wao kwake, wakati wa hafla ya kumpongeza kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati, iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, mkoani Mwanza, leo Ijumaa, tarehe 20 Juni 2025.

“Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia) kwa kuwa wewe ni Amiri Jeshi Mkuu, na sisi ni walinzi wako, watiifu kabisa, tunaomba upokee hadhi ya kuwa Mtemi wa Sungusungu. Nakukabidhi vifaa vya ulinzi wa jadi, ambavyo vitatolewa maelezo. Aidha, tunaomba tukutambulishe watemi na makamanda wa Sungusungu, ambao tumekuwa tukishirikiana katika mikoa hii mitano,” alisema Ndugu Richard Bundala, kiongozi wa Sungusungu hao.

Mtemi wa Sungusungu Kanda ya Ziwa, Sumbe Martine Mogani alimkabidhi Dkt. Samia silaha za kijadi, ambazo ni upinde na mishale, pamoja na mavazi ya kaniki na kofia, ikiwa ni ishara ya kumpatia heshima na hadhi hiyo ya kuwa mtemi wa Sungusungu katika mikoa hiyo mitano.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia aliwapongeza Sungusungu kwa kutimiza miaka 42 tangu jeshi hilo la ulinzi wa jadi lilipoanzishwa kwa nia ya kuitikia wito wa kisera wa ulinzi na usalama, uliomtaka kila Mtanzania kuwa mlinzi ndani ya nchi yake, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na mamlaka za kisheria, hasa Jeshi la Polisi, kupitia polisi jamii, katika kulinda amani na utulivu wa nchi katika maeneo yao.

Rais Dkt. Samia pia aliwapongeza walinzi hao wa jadi kwa mchango mkubwa ndani ya muda huo wote tangu kuanzishwa kwao, huku akiwataka kuendelea kuwa sehemu ya ulinzi na usalama wa mali na miradi ya maendeleo ambayo nchi imeanzishwa na kukamilishwa kwa gharama kubwa kote nchini.







Prev Post Nilifukuzwa Kwenye Kila Nyumba Niliyopanga Hadi Nilipoondoa Nuksi za Kifamilia Sasa Nina Nyumba Yangu Mwenyewe    
Next Post MAGAZETI ya Leo Jumamosi tarehe 21 June 2025
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook