
Ushindi wa Liverpool waleta balaa nchini Uingereza Jeshi la Polisi Merseyside limesema mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 53 amekamatwa baada ya gari kugonga watembea kwa miguu wakati wa gwaride la ushindi wa Kombe la Ligi Kuu ya England la Liverpool, na kusababisha watu wawili kujeruhiwa vibaya.
Watu 27 walikimbizwa hospitalini kwa gari la wagonjwa. Wawili kati yao — mmoja akiwa ni mtoto — walipata majeraha makubwa. Jumla ya watoto wanne walijeruhiwa.
Watu wengine 20 walitibiwa eneo la tukio na hawakuhitaji kupelekwa hospitalini. Mtaalamu wa huduma ya kwanza aliyekuwa kwenye baiskeli aligongwa na gari hilo lakini hakujeruhiwa.
Kulingana na Nick Searle, Afisa Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji wa Merseyside, wazima moto waliwaokoa watu wanne — wakiwemo mtoto mmoja — waliokuwa wamenaswa chini ya gari hilo.
Huduma za dharura ziliwasili haraka Water Street baada ya Polisi wa Merseyside kupokea taarifa kuhusu tukio hilo muda mfupi baada ya saa 12 jioni siku ya Jumatatu.
Gari hilo lilikomea eneo la tukio, na mwanaume kutoka eneo la Liverpool — anayeaminika kuwa dereva — alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi.
Naibu Kamishna Mkuu wa Polisi wa Merseyside, Jenny Sims, alisema tukio hilo halichukuliwi kama tendo la kigaidi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu jioni, alisema polisi wanaamini ni tukio la kipekee na kwa sasa hawamtafuti mtu mwingine yeyote kuhusiana nalo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!