
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, kulingana na matakwa ya Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, Serikali imetoa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za Mwaka 2025.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 2,2025 na Gavana wa BoT,Emmanuel Tutuba ambayo imefafanua kuwa,kanuni hizo zimechapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 198 la Machi 28, 2025.
“Kwa mujibu wa Kanuni hizo, bei na malipo ya bidhaa na huduma zote ndani ya nchi zinapaswa kufanyika kwa Shilingi ya Tanzania.
“Hivyo, ni kosa kunukuu, kutangaza au kubainisha bei kwa kutumia fedha za kigeni; kulazimisha, kuwezesha au kupokea malipo kwa fedha za kigeni au kukataa malipo kwa Shilingi ya Tanzania.”
Gavana Tutuba amefafanua kuwa,kanuni hizo pia zimeainisha miamala ambayo imeruhusiwa kufanyika kwa fedha za kigeni.
Aidha, Kanuni zimeweka ukomo wa muda kwa mikataba inayotekelezwa kwa fedha za kigeni na kuweka katazo la kutokuingia au kuhuisha mikataba inayotaka malipo yafanyike kwa fedha za kigeni kuanzia Machi 28,2025.
“Wageni kutoka nje ikiwemo watalii watabadili fedha za kigeni kupitia benki za biashara na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini au kuendelea kufanya malipo kwa kutumia kadi za kielektroniki au utaratibu wa kawaida wa kidigitali.
“Benki Kuu inawahimiza wananchi kutoa taarifa za ukiukwaji wa Kanuni hizi kupitia barua pepe: fx.regulations@bot.go.tz,Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU),Jeshi la Polisi, au mamlaka nyingine yoyote ya utekelezaji wa sheria kwa hatua stahiki.”
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!