
Hali ya kisiasa si shwari Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro baada ya kutokea vurugu na mashambulizi kabla ya kufanyika kuwa kura za maoni kwa wagombea wa nafasi ya ubunge katika Chama Cha Mapinduzi jmboni humo jana Jumapili..
Miongoni mwa matukio yaliyozua maswali mengi ni shambulio dhidi ya mke wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel, ambaye amedai gari lake lilivunjwa kioo na mkewe kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wasaidizi wa mmoja wa watia nia wa ubunge katika jimbo hilo.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Naibu Waziri Mollel amelipongeza Jeshi la Polisi Wilaya ya Siha kwa kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa watatu wanaohusishwa na tukio hilo, huku juhudi zikiendelea kuwatafuta wengine waliokimbia baada ya jaribio hilo la kushangaza.
Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo linahusishwa moja kwa moja na mchakato wa kisiasa ndani ya chama kutafuta mtu wa kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha Ubunge, ambapo mvutano mkali umeibuka miongoni mwa watia nia wanaowania kupitishwa na CCM kuwania nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu ujao katika jimbo hilo.
Bila kumtaja anayewania naye ubunge, Mollel alisema anawataka vijana wake wasichukue hatua yoyote na waachiwe vyombo vya dola vifanye kazi yake, “Hao watu wanataka kuvuruga uchaguzi ili uchaguzi katika jimbo hili usifanyika… naomba waliochoma moto gari wakamatwe kwa sababu kuna Ushahidi wa video…”alidai Mollel.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!