
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, ameonesha kutoridhishwa na mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili. Akieleza masikitiko yake mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu alidai kuwa kitendo kinachofanywa na mawakili wa serikali ni “kuendelea kuchelewesha haki.”
Akizungumza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Franco Kiswaga, Lissu amesema kesi hiyo imegeuzwa kuwa kitanzi cha kumuweka mahabusu akiwa na waliohukumiwa kifo bila sababu za msingi. Alisema hayo baada ya mawakili wa serikali kwa mara nyingine kuendelea kuomba kuahirishwa kwa kesi hiyo.
“Tunaendeshwa na mawakili wa serikali kwasababu mahakama yako imewaruhusu kuendeshwa na mawakili wa serikali…leo ni siku ya 112 tangu niwekwe mahabusu na wanataka ziendelee kuongezeka”.
Kauli ya Lissu imekuja baada ya upande wa Jamhuri kuieleza Mahakama kuwa bado haujawasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu kwa kuwa bado unasubiri uamuzi kuhusu maombi ya kulinda mashahidi. Wakili wa Serikali Mkuu, Nassor Katuga, amesema maamuzi hayo yanatarajiwa kutolewa na Mahakama Kuu tarehe 4 Agosti 2025.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Hakimu Kiswaga alisema. “Tukutane hapa tarehe 13 mwezi wa nane saa tatu asubuhi,” alisema huku akisisitiza kwamba hatapenda kusikia tena hoja za mawakili wa serikali zinazojirudia kila wakija mahakamani hapo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!