

Balozi Dkt. Shelukindo amesema hayo alipofungua Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO), Ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika nchini tarehe 21 hadi 25 Julai 2025, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

“Kanda yetu inapaswa kuendelea kuimarisha hatua za kukabiliana na vitisho vya kiusalama vinavyoendelea kuwepo, ambavyo vinatokana na uhalifu wa kimataifa uliopangwa, uhalifu wa mtandaoni, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na biashara haramu ya dawa za kulevya,”alisema Balozi Dkt. Shelukindo.
Ameongeza kuwa changamoto hizo zisipoangaliwa kwa umakini ni hatari kubwa kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya SADC ya mwaka 2050.

“Kutokana na hali hiyo Nchi wanachama zina jukumu la pamoja la kuimarisha mifumo ya kikanda inayolenga kuzuia na kupambana na uhalifu wa kimataifa uliopangwa”, alisisitiza Balozi Shelukindo.
Mkutano wa MCO ni miongoni mwa Mikutano ya ngazi za juu ya SADC, ambayo hufanyika mwezi Julai kila mwaka kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu amani, siasa na usalama katika nchi za ukanda wa SADC.

Mkutano huo unawakutanisha wajumbe wapatao 300 wakiwemo Mawaziri na Maafisa Waandamizi wanaoshughulikia masuala ya Mambo ya Nje, Ulinzi, Mambo ya Ndani na Usalama wa Umma kutoka Nchi Wanachama zote 16 za SADC.
Mkutano huo unafanyika nchini kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo katika Mkutano uliofanyika mwaka 2024 nchini Zimbabwe.

Nafasi hii muhimu imeiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mstari wa mbele katika kusimamia masuala yanayohusu amani, usalama na uthabiti wa kikanda kwa mujibu wa Itifaki ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Mkutano wa 27 wa MCO utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ambaye ni Mwenyekiti wa MCO na utafanyika tarehe 24 na 25 Julai 2025
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!