
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya imeondoa mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili mwanaharakati wa haki za binadamu Boniface Mwangi, na badala yake kumfungulia mashitaka mawili mapya.
Mwangi sasa anakabiliwa na tuhuma za kumiliki silaha bila kibali na kupatikana na sumu pamoja na vitoa machozi, madai ambayo aliyakana mbele ya mahakama. Aliachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja za Kenya.
Kukamatwa kwa Mwangi kumezua upinzani mkubwa kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu, yakidai kuwa ni njama ya kuzima sauti za ukosoaji dhidi ya serikali. Aidha mwanaharakati huyo alikana vikali mashtaka hayo kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), akisema, “Mimi si gaidi.”
Awali, serikali ilikuwa imemhusisha na maandamano ya kitaifa yaliyofanyika Juni 25, ambapo watu 19 waliuawa, mamia kujeruhiwa na mali kuharibiwa, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR).
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen, ameelezea maandamano hayo kama “ugaidi uliojificha kama upinzani” na alidai kuwa ni “jaribio la kuiangusha serikali kwa njia isiyo ya kikatiba.”
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!