
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis L. Londo (Mb. tarehe 18 Julai, 2025 ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia masuala ya Kilimo na Usalama wa Chakula.(SCAFS)
Mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri umefanyika jijini Arusha katika Makao Makuu ya EAC ambapo Mawaziri na viongozi mbalimbali kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameshiriki huku baadhi ya Mawaziri wa kushiriki kwa njia ya mtandao katika majadiliano yaliyohusa masuala anuai ikiwemo utekelezaji katika ngazi ya Jumuiya wa Maazimio ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Kampala kujadili Mpango Madhubuti wa Kuendeleza Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme – CAADP), Utekelezaji wa mipango ya pamoja ya maendeleo ya Kilimo na Mifugo hususan uhifadhi na usambazaji wa akiba ya chakula na mazao bora ya mifugo, kilimo cha mazao ya kipaumbele kwa ajili ya uhifadhi wa udongo ,usalama wa chakula na lishe bora.
Vilevile, Mkutano ulijadili kuhusu changamoto za upatikanaji wa vyanzo vya mapato kuendesha shughuli za kilimo na mifugo katika Jumuiya na matumizi sahihi ya fedha kuendesha shughuli hizo.
Aidha, Mkutano huo umepokea taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri, na Taarifa ya Jumla kuhusu Usalama wa Chakula na Lishe katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika kuhitimisha Mkutano husika, rai imetolewa kwa Wawakilishi wa Nchi Wanachama kuendelea kusisitiza Serikali zao kutekeleza wajibu wa kutoa Michango ya Uanachama ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za EAC kwa mujibu wa Bajeti iliyopitishwa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!