
Dar es Salaam, Tanzania – Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, aliyekuwa akiomba marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuahirisha usikilizwaji wa shauri linalomhusu.
Maombi hayo yalihusiana na kesi namba 8606/2025 ya uchapishaji wa taarifa za uongo mitandaoni, ambayo iliahirishwa tarehe 02 Juni 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Mhini. Kuahirishwa kwa kesi hiyo kulitokana na ombi la upande wa Jamhuri, uliotaka baadhi ya mashahidi ambao si askari wa Jeshi la Polisi watoe ushahidi wao kwa kificho.
Mahakama Kuu imeeleza kuwa maombi ya marejeo haya hayakuwa sahihi kwa wakati huu, kwani yalipaswa kusubiri hadi kesi ya msingi itakapokamilika ndipo yawasilishwe.
Wakili wa Lissu, Hekima Mwasipu, amesema kuwa sababu zilizoelezwa na upande wa Jamhuri kuomba ahirisho hilo hazikuwa na msingi wa kisheria, na kwamba hatua hiyo haikuwa sahihi. Hata hivyo, wamepokea uamuzi wa Mahakama Kuu kwa utulivu na kusisitiza kuwa endapo wataona umuhimu, watawasilisha tena maombi baada ya kesi ya msingi kuhitimishwa.
“Ahirisho la tarehe mbili la kutaka kusikiliza kesi halikuwa sahihi kwa sababu wao walileta sababu ambazo hazieleweki wala hazikuwa na misingi ya kisheria,” alisema Wakili Mwasipu.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!