

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, leo amefungua rasmi kikao kazi cha viongozi na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Kikao hicho muhimu kinawaleta pamoja viongozi waandamizi na watumishi wa TRA kutoka maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wa mamlaka hiyo katika mwaka uliopita wa fedha, kuainisha maeneo yaliyofanya vizuri, kubaini mapungufu, na kuweka mikakati thabiti kwa mwaka mpya wa fedha.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka viongozi wa TRA kuendelea kuwa na uwazi, uwajibikaji na ubunifu, akisisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ni mhimili muhimu wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.
“Niwapongeze kwa kazi kubwa mnayofanya lakini pia niwakumbushe kuwa bado tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mapato ya serikali yanakusanywa kwa ufanisi zaidi, bila kuwaonea au kubebesha mzigo wananchi wa kawaida,” alisema Majaliwa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!