Benki ya NMB imesema itaendelea kuwekeza kwenye mifumo ya kidijitali ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kupunguza utegemezi wa huduma za matawi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (DITF), Meneja Mwandamizi wa Mauzo Kidijitali wa benki hiyo Hezbon Mpate, alisema jukwaa la NMB Mkononi limekuwa chachu ya mageuzi ya sekta ya benki nchini, likiwawezesha mamilioni ya Watanzania kupata huduma za kibenki kwa urahisi, haraka na usalama.
“Kupitia NMB Mkononi, tumeweza kubadilisha namna Watanzania wanavyopata huduma za kifedha. Lengo letu ni kuhakikisha huduma zinapatikana kwa kila mtu, popote alipo, bila kikwazo cha umbali au muda,” alisema
Mpate alisema zaidi ya wateja milioni 4.7 wanatumia NMB Mkononi, na kwamba asilimia 96 ya miamala yote ya benki hiyo mwaka uliopita ilifanyika kwa njia za kidijitali, huku jukwaa hilo likipata ongezeko la matumizi kwa asilimia 16.
Alisema huduma hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano katika matawi ya benki na kuongeza ufanisi wa utendaji.
Katika kuhakikisha usalama wa miamala ya wateja, NMB imeanzisha matumizi ya alama za vidole (biometrics) kwa ajili ya kuingia na kufanya miamala kupitia programu hiyo.
Aidha, ukomo wa miamala ya kila siku umeongezwa kutoka Sh milioni 5 hadi Sh milioni 30 ili kutoa unafuu zaidi kwa wateja wanaofanya shughuli nyingi za kifedha. Kupitia huduma ya MshikoFasta.
Mpate alisema benki hiyo imefanikiwa kuwafikia wajasiriamali wadogo waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha. Huduma hiyo inatoa mikopo hadi Sh milioni moja bila dhamana, ndani ya dakika 10.
Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2022, zaidi ya mikopo milioni 3 imetolewa na kunufaisha karibu wateja milioni moja. “MshikoFasta imeleta suluhisho la kweli kwa mama lishe, machinga na watoa huduma wa kati. Kwao, dakika kumi zinaweza kuleta mabadiliko ya maisha,” aliongeza Mpate.
NMB pia imeanzisha huduma ya kisasa ya NMB Jirani Chatbot, inayopatikana kupitia WhatsApp, tovuti ya benki na mitandao ya kijamii. Kupitia mfumo huo, asilimia 78 ya maswali ya wateja hujibiwa papo kwa papo, hatua ambayo imepunguza maulizo yanayowasili katika vituo vya huduma kwa wateja kwa asilimia 22.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), asilimia 72 ya Watanzania wazima wanatumia huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali, huku idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu ikifikia zaidi ya milioni 38, na miamala ya kila mwezi ikikadiriwa kuwa zaidi ya Sh trilioni 14.
“Ahadi yetu ni kuendelea kuboresha NMB Mkononi ili kuwa jukwaa shirikishi zaidi, linalotoa huduma nyingi kwa urahisi, kwa usalama na kwa maisha bora ya wateja wetu,” alisisitiza
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!