Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imemteua Bw. Isack Nikodem Kihwili kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Bima ya Amana katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia tarehe 1 Agosti mwaka huu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Emmanuel Tutuba, ametangaza uteuzi huo na kusema DIB iko katika hatua za mwisho za kujitoa Benki Kuu ya Tanzania na kuwa taasisi inayojitegemea.
Uteuzi wa Bw. Kihwili ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Bodi hiyo unafuatia Serikali kuidhinisha muundo mpya wa taasisi hiyo.
“Kama sehemu ya utekelezaji wa muundo mpya ulioidhinishwa, Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Bima ya Amana imemteua Bw. Isack Nikodem Kihwili kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Bima ya Amana kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,” amesema Gavana Tutuba katika waraka wake kwa wafanyakazi wa DIB.
Bw. Kihwili anakuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa DIB.
Majukumu ya Bodi ya Bima ya Amana ni kutathmini na kukusanya michango kutoka benki na taasisi za fedha zinazopokea amana, na kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana, kukinga amana za wateja na kulipa fidia wenye amana endapo benki au taasisi ya fedha itaanguka au kufilisika.
DIB pia ina wajibu wa kufanya ufilisi wa benki au taasisi ya fedha iliyoshindwa kuendelea na biashara ya huduma za kibenki au iliyofilisika endapo ikiteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kama mfilisi. Aidha, kuanzia Julai mwaka huu, DIB imeongezewa jukumu la kushiriki katika kupunguza hasara kwa benki au taasisi ya fedha inayotetereka.
Bodi ya Bima ya Amana ilianzishwa kwa Mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Fedha ya mwaka 1991 na kuanza kufanya kazi mwaka 1994 kama idara ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, ikiwa na Bodi yake ya Wakurugenzi chini ya uenyekiti wa Gavana wa Benki ya Tanzania.
DIB inaendelea kufanya shughuli zake chini ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kwamba sasa iko katika hatua za mwisho kuwa taasisi inayojitegemea kama ilivyo kwa taasisi kama hizi duniani kote.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!