Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

TAMASHA LA SABASABA KUINUA UCHUMI WA UBUNIFU NA KUWEZESHA WASANII NA FAMILIA

  • 7
Scroll Down To Discover

Katika kuunga mkono juhudi za kukuza uchumi wa ubunifu na kutoa fursa kwa wasanii, wajasiriamali na familia kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni, Serikali imezindua rasmi Tamasha la Sabasaba kama sehemu muhimu ya Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) kwa mwaka 2025.

Akizungumza leo Juni 29, 2025 Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema tamasha hilo, ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu, linatarajiwa kuwa kivutio kikuu kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo, huku likiwa jukwaa mahsusi kwa wasanii na wadau wa sekta ya ubunifu kuonesha na kuuza kazi zao.

“Tamasha hili si tu linatoa burudani, bali pia limejikita katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii, ikiwa ni pamoja na usajili wa kazi za sanaa, utoaji wa mikopo kwa wasanii, kusajili vyama vya michezo na kutoa vibali vya shughuli za filamu,” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa tamasha hilo, linalofanyika katika eneo maalum la zaidi ya ekari moja lililotengwa na TANTRADE, linaangazia pia urasimishaji wa sekta ya sanaa kupitia huduma kama Press Cards kwa waandishi wa habari, usajili wa magazeti, leseni kwa wasanii na huduma nyingine za papo kwa papo.

Kwa upande wa burudani, Msigwa amesema kutakuwa na muziki wa aina mbalimbali kama Singeli, Bongoflava, Taarabu na muziki wa dansi, pamoja na maonyesho ya mavazi kutoka kwa wanamitindo maarufu akiwemo Anna Collection. Pia kutakuwa na uwepo wa wasanii mahiri kama Alikiba, Lady Jaydee, Nandy, Jacquiline Wolper, Kombolela, na wengine wengi walioandaa mabanda ya kuonesha kazi na bidhaa zao.

“Tamasha hili linawawezesha wananchi si tu kuburudika, bali pia kujifunza, kuuliza maswali na kushiriki moja kwa moja na wasanii wanaowapenda. Hili ni jukwaa la maingiliano ya moja kwa moja kati ya jamii na wadau wa sanaa,” amefafanua Msigwa.

Aidha, amesema tamasha hilo pia limeweka mazingira rafiki kwa familia, likiwa na michezo ya watoto ili kuwawezesha kupata burudani wakati wa likizo, huku akiwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kushiriki katika kijiji hicho cha burudani.

Kwa ujumla, Tamasha la Sabasaba limejipambanua kama sehemu muhimu ya kukuza vipato vya wasanii, kuchochea ubunifu, na kuongeza ushiriki wa jamii katika Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam, likiunganisha biashara, utamaduni, sanaa na familia kwa pamoja.



Prev Post Equatorial Guinea: Baltasar Engonga Atupwa Jela Miaka 18 kwa Ubadhirifu
Next Post HEINEKEN SILVER YAPOKELEWA KWA SHANGWE 
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook