Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Serikali Yakanusha Madai ya Njama ya Kumuua Tundu Lissu kwa Sumu

  • 8
Scroll Down To Discover

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Julai 3, 2025 imekanusha vikali madai yanayosambaa mitandaoni na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu kuwepo kwa njama ya kumtilia sumu kiongozi wa chama cha upinzani CHADEMA, Tundu Antipas Lissu, ambaye kwa sasa anashikiliwa rumande akisubiri uamuzi wa mashauri yake mahakamani.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, Serikali imeeleza kuwa madai hayo ni ya “uzushi, hayana msingi wowote, na yana lengo ovu la kuchafua sifa ya Tanzania kitaifa na kimataifa.”

“Serikali inawaomba wananchi wapuuze taarifa hizo kwa kuwa hazina ukweli wowote. Tundu Antipas Lissu anakabiliwa na mashtaka mahakamani kwa mujibu wa sheria, na anashikiliwa gerezani hadi hapo shauri lake litakapohitimishwa na Mahakama,” alisema Msigwa.

Ameongeza kuwa Serikali haijawahi, na haina mpango wowote wa, kumdhuru mtu yeyote aliyeko kizuizini na kwamba taarifa hizo ni sehemu ya kampeni chafu za kisiasa zinazoendeshwa kwa lengo la kuichafua Tanzania mbele ya macho ya dunia.

Taarifa ya Serikali inakuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoa taarifa rasmi kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, ambapo kilieleza hofu juu ya usalama wa Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, anayeshikiliwa kwa tuhuma mbalimbali.

“CHADEMA kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa zinazodai kuwa kuna mipango ya kumuwekea sumu Mhe. Tundu Lissu akiwa kizuizini,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya chama hicho cha upinzani.

Chama hicho pia kilinukuu kauli ya David McAllister, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya, ambaye kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), aliandika:

“Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kutisha za jaribio la kumtilia sumu kiongozi wa upinzani wa Tanzania, Tundu Lissu, akiwa kizuizini.”

CHADEMA imeitaka Serikali kutoa uhakikisho wa usalama wa Lissu, na kutaka uchunguzi huru kuhusu madai hayo, sambamba na wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kesi na mazingira ya kushikiliwa kwa kiongozi wao.



Prev Post Shigongo Azindua Kivuko Cha MV Mwanza, Aishukuru Serikali kwa Kuimarisha Usafiri Buchosa
Next Post Waziri Paramagamba Kabudi Alivyofika Banda la NIC Sabasaba Kujionea
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook