

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, amewashutumu baadhi ya raia na wanasiasa wa nchi hiyo wanaotafuta msaada wa kisiasa nje ya taifa hilo, akidai kuwa tabia hiyo inaonesha kutokujua maana halisi ya uhuru.
Akizungumza jana Jumanne, Julai 1, 2025, katika maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Burundi, Rais Ndayishimiye amesema: “Mrundi yeyote ambaye ana tatizo nchini na kwenda nje ya nchi kutafuta suluhisho, ni kwamba bado hajajifunza uhuru ni nini.”
Rais Ndanyishimiye amewalinganisha wanasiasa hao na wanachama wa chama cha PDC kilichopinga uhuru wa Burundi mwaka 1962 na kutaka watawala wa kikoloni waendelee.
Bila kuwataja majina moja kwa moja, Rais Ndayishimiye ameonekana kuwalenga wanasiasa wa upinzani waliokimbilia uhamishoni, waliotangaza hivi karibuni mpango wa kuanzisha harakati za silaha wakipinga matokeo ya uchaguzi wa bunge na manispaa uliofanyika hivi karibuni.
“Wana roho ya PDC… wamepoteza uchaguzi, halafu wanaenda Umoja wa Mataifa au Umoja wa Afrika kutafuta msaada. Je, wao ndio watakaowapigia kura?” amehoji Rais.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya viongozi wa makundi ya upinzani yaliyo uhamishoni kutangaza rasmi, mjini Brussels Ubelgiji, kuwa wameamua kuanza mapambano ya silaha baada ya kile walichokiita wizi wa kura na kushindwa kwa njia za amani.
Frederique Bamvuginyumvira, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Burundi, alisema: “Tumeona uchaguzi ukiibiwa waziwazi… tumepuuzwa kwenye mazungumzo zaidi ya mara nane. Sasa tumeamua kupigana – si kwa chuki, bali kwa ajili ya ukombozi.”
Makundi yanayohusika ni pamoja na CFor-Arusha, CN (Coalition for the Renaissance of the Nation), na Patriotic Action Movement. Ingawa hawakutaja kundi litakalotekeleza harakati za kijeshi, walidai kuwa wanaungwa mkono kutoka ndani na nje ya nchi.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!