

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, amesema kuwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ikiwemo kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi wakati wa ibada, zinaathiri taswira ya taifa na ni ukiukwaji wa haki ya msingi ya kuabudu.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya mtandaoni ya Saut Digital, Askofu Bagonza amesema kuwa kama kuna tatizo na Askofu aliyelianzisha kanisa, basi hatua zichukuliwe dhidi yake binafsi na si kuwakandamiza waumini wanaokusanyika kwa ibada.
“Kama tatizo ni la Askofu aliyeanzisha kanisa, kamateni yeye sukuma ndani, lakini watu wapewe uhuru wao wa kuabudu. Hii picha inayojitokeza ya kupiga mabomu watu wanaoabudu haina faida kwa yeyote,” amesema.
Kauli hiyo imekuja baada ya tukio la Jumapili lililohusisha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwatawanya waumini waliokuwa wakikusanyika kwa maombi eneo la Ubungo Kibo, kwa kutumia mabomu ya machozi, huku watu 52 wakikamatwa kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko haramu na kuchochea vurugu.
Askofu Bagonza ameonya kuwa hatua kama hizo hazitasaidia kulinda amani, bali zinaweza kuchochea hisia za hasira miongoni mwa wananchi.
“Ni wiki ya tatu sasa Jumapili watu wanapigwa mabomu wakati wanaabudu. Wasifikiri kimya cha watu kinakubaliana na matendo haya. Hapana. Watu wengi wamechukia mpaka hawataki hata kusema,” ameongeza.
Katika taarifa ya polisi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne Muliro, ilieleza kuwa waliokamatwa walifanya fujo na jaribio la kuingia kwenye barabara yenye magari mengi kwa lengo la kuchochea taharuki, hatua ambayo ni kinyume na sheria.
Polisi pia wametoa onyo kwa wananchi kuzingatia sheria na kuepuka mikusanyiko isiyoruhusiwa kisheria.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!