

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Benki Kuu pamoja na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kupitia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya fedha kimataifa na kiinchi ili kulinda na kuepuka hatari ya kupoteza rasilimali.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Maadhimisho ya Miaka 30 ya Benki ya CRDB pamoja Semina ya Wanahisa wa Benki hiyo inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Amesema matumizi makubwa ya teknolojia yanaondoa mipaka ya kijiografia na hivyo kuunganisha huduma za fedha duniani hivyo ni muhimu kuwepo na menejimenti ya vihatarishi na hitaji la kuzingatia kanuni za kifedha za kimataifa.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa Benki ya CRDB kuweka mkazo zaidi katika udhibiti wa tishio la uhalifu wa kimtandao ili kujenga imani ya wateja na kulinda heshima ya benki hiyo. Amesema Benki ya CRDB haina budi kujihami mapema na wakati wowote kwa sababu, kukua kwa matumizi ya teknolojia kumeleta wimbi la matukio ya uhalifu wa kimtandao unaohatarisha mitaji ya benki duniani na kuongeza gharama za kukabiliana nao.
Aidha Makamu wa Rais amesema ni vema kuendelea kufanya mageuzi ya kiteknolojia kwa kuongeza matumizi ya huduma za kimtandao ili kuongeza ufanisi, usalama, na ushindani. Amewasihi kufanya ushirikiano na wadau wa teknolojia ya fedha ili kubuni bidhaa na huduma zenye ubora. Amesema kuwekeza kwenye Teknolojia kutapunguza gharama za uendeshaji, kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi hususan walio vijijini na maeneo yasiyo na matawi na kwa watu wenye kipato cha chini au wasioweza kufungua akaunti za kawaida.
Katika kulinda mazingira, Makamu wa Rais ametoa rai kwa mabenki kuangalia uwezekano wa kuunganisha nguvu kwa kuwa na miradi ya pamoja na Taasisi nyingine za fedha, ili kupata kiwango kikubwa zaidi cha fedha na kuziba pengo la ufadhili wa miradi ya mazingira ambalo bado ni kubwa mno.
Makamu wa Rais amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi. Amesema Serikali imeboresha sera na kuweka mifumo madhubuti, imejenga miundombinu wezesha na imeendelea kukuza uchumi wa nchi na kipato cha wananchi.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!